*********************
NA EMMANUEL MBATILO
Serikali imezitaka Halmashauri nchini, kuhakikisha zinajenga miundombinu yake kwa mapato ya ndani, badala ya kusubiri ruzuku serikali kuu.
Akizungumza katika ziara yake ya kikazi ya kutembelea miradi mbalimbali wilayani Ilala jijini Dar es Salaam,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe.Selemani Jafo ameagiza Wakala wa Barabara, Mjini na Vijijini (TARURA), kuanza ujenzi wa barabara kuu ya Vingunguti inayounganisha barabara ya Nyerere na kuhakikisha kukamilika kwake kunaenda sambamba na kukamilika kwa machinjio.
Alisema Wilaya ya Ilala imekua mfano mzuri kwa ujenzi wa miundombinu yake kwa kutumua mapato yake ya ndani ikiwemo Hospitali Kuu ya wilaya hiyo, Shule ya Msingi na Sekondari Magole.
Alisema Wilaya hiyo inaongoza kwa ukusanyaji wa mapatoya ndani ambapo Hadi mwezi Septemba mwaka jana ilikusanya sh. bilioni 29.07.
Akiwa katika mradi wa Machinjio ya Vingunguti Jaffo, aliiagiza ujenzi huo kuendelea kwa kasi Kama ilivyo sasa na kuhakikisha unakabidhiwa siku iliyoahidiwa ambayo ni Julai 17, mwaka huu.
Alimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Jumanne Shauri, kuhakikisha anatenga eneo kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo, waliokuwa katika machinjio ya zamani, ili wapate nafasi na kuendelea na biashara zao.
“Machinjio mapya yanatarajiwa kuwa mkombozi wa wananchi katika biashara na shughuli mbalimbali hivyo ni vyema Mkurugenzi akatafuta eneo haraka kwa ajili ya wafanyabiashara hao ili machinjio yakikamilika yasiwe sababu ya wao kukosa nafasi,” alisema.
Alitoa siku 13, Hadi Machi 15 kuanzia Leo kwa Mkurugenzi huyo kutafuta eneo na lianze kuandaliwa.
Pia Mhe.Jaffo, alieleza kuridhishwa na ubora wa mradi pamoja na kasi ya ujenzi wa usiku na mchana.
Aidha alimtaka Mtendaji Mkuu wa TARURA jijini Dar es Salaam, kutuma kikosi kazi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara ya Vingunguti ili ikamilike sambamba na kukamilika kwa machinjio hayo.
Alisema barabara hiyo ndio njia kuu kuelekea machinjio hayo hivyo ni budi kuikamilisha ili isiwe kikwazo kwa wafanyabiashara katika kufika katika machinjio hayo.
Kuhusu Hospitali ya Ilala Mhe.Jaffo, aliagiza ujenzi huo kukamilika kufikia Mei 30, mwaka huu.
Pia alipotembelea ujenzi wa Shule ya Sekondari Magole, alimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo afanye busara za kuzungumza na Mzee wa miaka zaidi 100 anayelalamikia kuwa eneo ilipojengwa shule ni lake.
Pia alisema kama Kuna maamuzi yoyote yanahakama yeye Hana mamlaka ya kuyaingilia