*****************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea taarifa ya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali katika tasnia ya kilimo cha mkonge mkoani Tangana kuagiza mapendekezo yaliyotolewa na timu hiyo yakiwemo ya kurejeshwa Serikalini kwa nyumba na. 176 eneo la Bombo ambayo ilimilikishwa kwa Bw. Salum Shamte yafanyiwe kazi.
Nyumba nyingine zilizopendekezwa kurejeshwa Serikalini ni pamoja na nyumba kumi zilizoko ndani ya Jiji la Tanga katika maeneo ya Raskazone, Bombo, Nguvumali na Market street ambazo zilinunuliwa na watumishi hao kwa udanganyifu.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumapili, Machi 1, 2020) wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri za mkoa wa Tanga, viongozi wa taasisi mbalimbali, wadau wa zao la mkonge pamoja na viongozi wa dini kwenye ukumbi wa hoteli ya Naivera.
Hata hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wawekezaji ambao wanamiliki mashamba ya mkonge yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 2,000 ambao hawajayaendeleza wayaendeleze wakishindwa yatachukuliwa na kugawiwa kwa wananchi.
Timu hiyo maalum ya uchunguzi iliundwa na Waziri Mkuu na ilifanya uchunguzi mkoani Tanga kuanzia tarehe 29/11/2019 hadi tarehe 07/02/2020. Timu hiyo iliyokuwa na wajumbe 13 ilihusisha maafisa kutoka ofisi mbalimbali za Serikali.
Uchunguzi huo maalum ulihusu masuala mbalimbali katika tasnia ya zao la mkonge mkoani Tanga ambayo ni pamoja na uzalishaji wa mkonge, bei ya zao la mkonge katika soko la ndani na nje ya nchi.
Pia, ilichunguza kuhusu mali za iliyokuwa Mamlaka ya mkonge nchini, ubia kati ya Kampuni ya Katani Limited na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Utendaji kazi wa Kampuni ya Katani Ltd na pia Utendaji kazi wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB).
Awali,Mwenyekiti wa timu hiyo Bw. Gerald Kusaya alisema timu ilibaini kuwa Kampuni ya Katani Ltd tokea mwanzo ilikuwa na mgongano wa kimaslahi na kupelekea kuhujumu uchumi kwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wake Bw. Salum Shamte alikuwa mtumishi wa umma na alishiriki vikao vyote vya ubinafsishaji wa Mamlaka ya Mkonge ilhali akijua kuwa ana maslahi kwenye Kampuni inayonunua.
“Kwa kuwa uchunguzi umebaini viongozi na wanahisa wa Katani Ltd waliohusika kuingia mikataba walikuwa watumishi wa Mamlaka ya Mkonge wakati wa mchakato wote wa ubinafsishaji hivyo walitumia vibaya madaraka yao kwa kuishawishi Serikali kuingia mkataba huo usiokuwa na tija kwa Serikali bali kwa manufaa yao binafsi. Hivyo, Timu imeandaa taratibu kwa ajili ya wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.”
Bw. Kusaya amesema timu hiyo inapendekeza kuwa Serikali itoe fedha kwa ajili ya kazi ya kuyapima upya mashamba matano ya Mwelya, Ngombezi, Hale, Magunga na Magoma ili wananchi wanaoendelea kutumia mashamba hayo kwa kukodishwa na Bodi ya Mkonge kama ilivyokubalika kwenye Baraza la Mawaziri mwaka 2005 ili waweze kupewa Hati ndogo (leasehold tittle);
Alisema timu inapendekeza nyumba 30 zilizopo eneo la Muheza, ambazo baadhi zilitolewa kwa wananchi waliokuwa watumishi wa Mamlaka ya Mkonge na baadhi kuachwa kwa ajili ya makazi ziendelee kuwa mali ya wananchi hao kwa kuwa eneo hilo kwa sasa lipo chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Muheza.
“Nyumba 22 zilizoko ndani ya mashamba ya mkonge na maeneo ya kiwanda cha TANCORD ziendelee kubaki mali ya Serikali na nyumba iliyoko katika kiwanja Na. 176 eneo la Bombo iliyohamishwa kwenda kwa Ndg. Salum Shamte irejeshwe Serikalini kwa njia ya urekebishaji wa daftari la Msajili wa Hati.”
Kwa upande wao, viongozi wa mkoa wa Tanga wakiwemo wabunge wamemshukuru Waziri Mkuu kwa kuunda timu hiyo ya uchunguzi wa zao la mkonge kwa kuwa mapendekezo yake yamejibu changamoto zilizokuwa zinalikabili zao hilo.
Wamesema mapendekezo yaliyotolewa na timu hiyo yanakwenda kufufua kilimo cha zao la mkonge hivyo kuongeza tija kwa wakulima wa mkonge mkoani Tanga.