KILI MARATHON 2020: Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangalla akishiriki mbio za Kili Marathon ( KM 21) mjini Moshi leo.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangalla akitoa nishani na zawadi kwa washindi wa Kili Marathon 2020 leo mjini Moshi.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla akionesha Nishani aliyopewa mara baada ya kumaliza mbio za Kilometa 21 kwenye mbio za Kili Marathon leo mjini Moshi.
****************************
Na. Aron Msigwa – WMU, Moshi.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.Hamisi Kigwangalla ametoa wito kwa Watanzania hususani vijana wajitokeze kushirikimashindano mbalimbali yanayofanyika nchini Tanzania yakiwemo ya Kilimanjaro Premium Lager Marathon ili wanufaike wanufaike kiuchumi.
Dkt. Kigwangalla ameyasema hayo mjini Moshi wakati akizungumza na wakazi wa mji wa Moshi na maelfu ya wakimbiaji waliojitokeza kushiriki Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon mwaka 2020 katika uwanja wa Michezo wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.
Dkt. Kigwangalla ambaye alikua mgeni rasmi na miongoni mwa washiriki wa mbio hizo kwa upande wa Kilometa 21 amesema ushiriki wa Watanzania katika mbio za KILI Marathon unachangia kuimarisha afya za washiriki na kutoa fursa ya ajira kwa wakimbiaji, kukuza kipato kwa wenyeji kufanya biashara na kuuza huduma mbalimbali kwa wageni.
Dkt. Kigwangalla amewashukuru waandaji wa mbio hizo ambazo zimejumuisha washiriki zaidi ya elfu kumi na mbili (12,000) kutoka nchi zaidi ya 56.
Amesema ujio wa wageni hao kutoka mataifa mbalimbali ni fursa ya kiuchumi kwa Watanzania pia ni moja ya mkakati wa kukuza na kutangaza vivutio mbalimbali vya Utalii.
” Unapopata wageni kutoka nchi zaidi ya 56 kwa wakati mmoja ni jambo la kujivunia, sio jambo dogo sisi kama wizara tumelichukulia kwa uzito mkubwa na ndio maana niko hapa leo pamoja na watendaji kutoka Taasisi mbalimbali kama vile Bodi ya Utalii , TANAPA, KINAPA , Ngorongoro na wadau wengine wa utalii ili kwa pamoja tutangaze utalii uliopo nchini kwetu” Amesema Dkt. Kigwangalla.
Ameeleza kuwa washiriki wa mbio hizo pamoja na mambo mengine wanapata fursa ya kuzuru vivutio vya utalii ikiwemo kupanda Mlima Kilimanjaro , kutembelea eneo la Ngorongoro, Zanzibar, Mikumi Ruaha, Nyerere na maeneo mengine yenye vivutio vya utalii na kuchangia katika kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa.
” Watalii hawa hufanya matumizi mbalimbali wanapotembelea vivutio vyetu na hii hukuza biashara mbalimbali, ni jambo la kuungwa mkono kwa nguvu zote natoa rai kwa waandaaji tuendelee kushirikiana pamoja na Wizara ya Habari , Utamaduni, Sanaa na Michezo ili tusukume gurudumu hili” Amesisitiza Dkt.Kigwangalla.
Dkt.Kigwangalla ametoa wito kwa watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya utalii.
” Tumeshusha viingilio kwa kiasi kikubwa ili Watanzania wengi zaidi wapate fursa ya kutembelea vivutio hivi na hii ni pamoja na wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi vyuo, Tutumie fursa hii vizuri na Wizara yangu itagakikisha vivutio vyote vinakuwa katika hali ya ubora unaotakiwa ” Amesisitiza Dkt. Kigwangalla.
Aidha, amewataka waandaaji wa mbio mbalimbali zinazovutia watalii wajitokeze na kuishirikisha Wizara ili isaidie kuweka mikakati mizuri ya matumizi ya fursa zilizopo.
Amesema Serikali itaendelea kuunga mkono mashindano hayo na kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara ili mashindano hayo yaendelee kuwa kivutio miongoni mwa washiriki, yakuze utalii na kuwa chanzo kikubwa cha mapato.
Kwa Upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza wakati wa utoaji wa Nishani na zawadi mbalimbali kwa Washindi wa mbio hizo ametoa wito kwa waandaji wa mbio hizo wawahamasishe vijana wa Kitanzania washiriki mashindano hayo na kushinda Tuzo na zawadi mbalimbali zinazotolewa badala ya kuachia wageni.
Dkt. Mwakyembe ametoa rai hiyo kufuatia idadi kubwa ya washindi wa nafasi za juu katika mashindano hayo kuwa wageni kutoka nchi za jirani za Kenya na Uganda.
Amesema Tanzania ina vijana wazuri wenye uwezo wa kukimbia na kupeperusha bendera ya Tanzania Kimataifa akibainisha kwamba jambo hilo la ushiriki hafifu wa Watanzania katika mashindano ya Marathoni lazima litafutiwe ufumbuzi.
” Haiwezekani, Tanzania tunao vijana wazuri sana na wenye uwezo wa kukimbia kwa spidi kama ya pikipiki, hatuwezi kuendelea kuwaachia wageni ndio wakawa wanashika nafasi za kwanza na kuchukua fedha wakati vijana wa kitanzania miguu mnayo na uwezo wa kukimbia mkachukua fedha hizi upo” Amesisitiza.
Kufuatia hali hiyo ametoa agizo kwa viongozi wa mchezo wa riadha kutoka maeneo mbalimbali nchini kukutana naye mjini Dodoma ili waweze kufanya maamuzi juu ya hiyo hilo.
Aidha amesema kuwa Wizara yake itaendelea kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuweka miundombinu na mazingira wezeshi ya kuongeza idadi ya washiriki wanaojitokeza katika mashindano hayo ikiwemo ujenzi wa miundombinu na njia maalum zitakazoongeza idadi kubwa ya wakimbiaji wa Kili Marathon kutoka katika mataifa mbalimbali.