Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Mussa Zungu akipanda mti katika Uzinduzi wa Kampeni ya Upandaji miti iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Shabani Robert Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Mussa Zungu (kushoto mwenye kofia) akipata maelekezo na Mwanzilishi wa Mradi wa KopaGas katika Kampeni ya Upandaji Miti iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Shabani Robert Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Mussa Zungu akizungumza na Wadau Mbalimbali katika Kampeni ya Upandaji Miti iliyofanyika Katika Shule ya Sekondari Shabani Robert Jijini Dar es Salaam.
***************************
NA EMMANUEL MBATILO
Serikali itaweka mpango kwa kila kaya kuhakikisha inapanda mti hata mmoja na kuhamasika kutumia nishati mbadala, ili kukabiliana na athari zinazotokana na uharibifu wa mazingira katika jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza katika Uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti ya Asasi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na shughuli za utunzaji wa mazingira (ALSF), Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mussa Zungu, alisema kwa kutumia mfumo huo mpandaji wa mti atalazimika kuuhudumia.
Aidha, Mhe.Zungu alisema kuwa itakavyokuwa kwa mfumo huo ni kwamba, mti utakuwa chini ya umiliki wa mtu mwingine ambaye atahusika kufuatilia maendeleo yake popote alipo kwa njia ya video huku muhudumu wa mti huo ataendelea kuutunza na kulipwa fidia.
“Hivi karibuni mtu atakuwa anapanda mti na kuuhudumia chini ya uangalizi maalumu kwamba ukiupanga kutakuwa na mtu anayefuatilia ukuaji wake kwa njia ya video na anayeuhudumia atalipwa fidia,” alisema Mhe.Zungu.
Pia Mhe.Zungu alisema kuna mpango uliopo wa kuhamasisha upandaji wa mti kwa kila kaya jijini Dar es Salaam, ili kuondoa changamoto za kimazingira zinazosababishwa na uchache wa uoto wa asili jijini humo.
Alisema mkoa wa Dar es Salaam ndio kinara kwa matumizi ya mkaa ambapo mwaka 2011 pekee ilitumia tani milioni moja za mkaa ambazo ni sawa na uharibifu wa hekta 1,10,000 za miti.
Alizitaka kampuni za gesi kupunguza gharama za nishati hiyo ili jamii ihamasike kutumia nishati mbadala na kuacha kutumia mkaa.
“Wauzaji wa nishati ya gesi ni vyema mpunguze gharama za nishati hiyo kwani hata kwa viwango vya dunia imepungua hii itasaidia watu kuachana na matumizi ya mkaa kama nishati ya kupikia.
Aliongeza kuwa inakadiriwa kuwa mkoa wa Dar es Salaam baada ya miaka saba kutakuwa na wakazi milioni 10, hivyo kampuni za gesi ziboreshe miundombinu yake ili kuwa na nishati hiyo itakayokidhi idadi ya watu hao.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Asasi ya ALSF Thomas Mchiwa, aliiomba serikali kuwasaidia kufanikisha kampeni ya upandaji wa miti ili kuwa na mazingira bora nchini.
Alisema ni vyema kila jumamosi ya usafi iambatane na shughuli za utunzaji wa mazingira ikiwemo upandaji wa miti, kila nyumba ihakikishe inapanda mti hata wa matunda.
Naye Mkurugenzi wa Kopa Gas, ambaye pia ndiye mbunifu wa matumizi ya gesi kwa njia ya kielektroniki, Andron Mendez, alisema teknolojia hiyo inalenga kurahisisha gharama za matumizi ya nishati hiyo.
Alisema badala ya mtumiaji kulazimika kununua mtungi mzima wa gesi sasa atakuwa na uwezo wa kujaza gesi kulingana na thamani ya fedha aliyonayo popote alipo.
Aliongeza kuwa teknolojia hiyo inaweza kujaza gesi hadi ya sh. 500, popote mteja alipo.