YANGA SC imepata ushindi wa kwanza katika mechi tano za Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Alliance FC ya Mwanza mabao 2-0 usiku wa leo Uwanja wa Taifa Jijini es Salaam.
Ushindi huo unaofuatia sare nne mfululizo, unaifanya Yanga SC ifikishe pointi 44 baada ya kucheza mechi 23, ingawa inabaki nafasi ya tatu sasa ikizidiwa pointi moja tu na Namungo FC inayoshika nafas ya tatu, ambayo hata hivyo imecheza mechi moja zaidi.
Shujaa wa Yanga SC katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Omary Mdoe aliyesaidiwa na Mohamed Mkono na Arnord Bugado wote wa Tanga ni mshambuliaji wake mpya, Dtram Adrian Nchimbi aliyefunga mabao yote mawili baada ya kutokea benchi kipindi cha pili.
Nchimbi aliyechukua nafasi ya mchezaji mwenzake mpya, Tariq Seif Kiakala alifunga mabao yake dakika ya 47 akimalizia pasi ya winga Mghana, Bernard Morrison na 78 baada ya kuuwahi mpira mrefu ulioanzishwa na kipa Metacha Boniphace Mnata.
Hata hivyo, baada ya mabao hayo mawili, Yanga SC walionekana kuridhika na kucheza kwa kuwafurahisha mashabiki wao badala ya kutafuta mabao zaidi.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Metacha Mnata, Juma Abdul, Jafary Mohammed, Lamine Moro, Said Juma ‘Makapu’, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Deus Kaseke/Mapinduzi Balama dk74, Haruna Niyonzima, Tariq Seif/Ditram Nchimbi dk46, Erick Kabamba/Mohamed Issa ‘Banka’ dk54 na Bernard Morrison.
Alliance FC; Andrew Ntala, Godlove Mdumule, Mackenzie Ramadhani, Joseph James, Geoffrey Luseke, Shaaban William, Martin King, Juma Nyangi, David Richard, Sameer Vincent na Deus Cosmas.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, bao la dakika ya 90 la mshambuliajii chipukizi, Andrew Simchimba limetosha kuipa Azam FC ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya wenyeji, JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Kwa ushindi huo, Azam FC inayofundishwa na Mromania, Aristica Cioaba inafikisha pointi 48 baada ya kucheza mechi 25, hivyo kuendelea kushika nafas ya pilim, nyuma ya mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 62 za mechi 24.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Namungo FC imeshinda 2-1 dhidi ya Lipuli FC Uwanja wa Samora mjini Iringa hivyo kufikisha pointi 46 katika mchezo wa 24 na kuendelea kukamata nafas ya tatu, mbele ya Yanga yenye pointi 41 za mechi 22.
Nayo Ruvu Shooting imeibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Mbao FC, mabao ya Graham Naftal na Baraka Mtuwi Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Mwadui FC imeshinda 2-0 dhidi ya Coastal Union, mabao ya Raphael Aloba dakika ya 19 na Mussa Chambega dakika ya 82 Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Mtibwa Sugar nayo ikaibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Ndanda FC, mabao ya Juma Luizio dakika ya 10 na Haroun Chanongo dakika ya 85 Uwanja wa CCM Gairo mkoani Morogoro.
Biashara United 1 nayo ikaibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara bao pekee la Lenny Kissu.
Kagera Sugar ikalazimishwa sare ya 1-1 na Tanzania Prisons Uwanja wa Kaitaba mjin Bukoba, wakati Singida United ikachapwa 1-0 na Polisi Tanzania, bao pekee la Sixtus Sabilo kwa penalti dakika ya 62 Uwanja wa Liti, zamani Namfua mkoani Singida.