Muonekano wa Machinjio iliyofungwa na TBS Mkoa wa Singida
Mfereji wa eneo la machinjio unaotiririsha maji taka hadi kwenye makazi ya watu.
Maofisa wa TBS kutoka Kanda ya Kati wakifanya ukaguzi kwenye machinjio hayo. |
Muonekano wa maji taka yanayosambaa hovyo kwenye machinjio hiyo.
Afisa wa TBS Kanda ya Kati, Vincent Mileo akizungumza.
Afisa wa TBS Kanda ya Kati, Maua Said akizungumza .
Mkazi wa eneo la Mitunduruni ilipo machinjio hiyo, Jumanne Ramadhani akizungumza.
Karo la mizoga lililoharibika na kusababisha harufu kali.
Mwonekano wa maji taka yanayosambaa hadi kwenye makazi.
Mwonekano wa mfereji unaotiririsha maji taka.
Na Ismail Luhamba, Singida
SHIRIKA la Viwango Nchini (TBS) hatimaye imefunga machinjio ya nyama iliyopo Kata ya Muhan’ga, Manispaa ya Singida mkoani hapa kutokana na kushindwa kuendeshwa kwa kuzingatia vigezo stahiki kwa afya na usalama wa mlaji.
Akizungumza mara baada ya kufunga machinjio hayo jana, Afisa Usalama wa Chakula kutoka Kanda ya Kati, Vincent Mileo, alisema wameamua kufunga machinjio hayo mpaka hapo marekebisho yote stahiki yatakapofanyika
“Wananchi kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamika, na tulipofika hapa kweli tumebaini kuna kasoro zikiwemo kutiririsha maji machafu kwenye makazi ya watu, mfumo wake wa maji taka ni mbovu, makaro yamepasuka na yanatoa harufu kali sana ambayo ni kero kwa wakazi wanaozunguka maeneo yote ya machinjio,” alisema
Kwa upande wake, Afisa wa TBS Kanda ya Kati, Maua Said, alisema kwa hali halisi waliyoiona eneo hili ni dhahiri kuna viashiria vyote vinavyoweza kusababisha mlipuko wa magonjwa mbalimbali
“Kuna kwa hali ilivyo hapa ni rahisi sana wakazi hawa wakaweza kupata magonjwa yanayoweza kutoka kwa mnyama kwenda binadamu, mathalani TB kutokana na kupasuka kwa shimo hili la kutupia mizoga ambalo linatoa harufu kali sana,” alisema Maua Said
Hata hivyo mmoja wa wakazi wa eneo hilo Jumanne Ramadhan, alisema wapo mbioni kuhakikisha wanapeleka suala hilo mahakamani ili kuomba mashinjio ihamishwe au kama itashindikana basi wakazi hao wahamishwe ili kuepuka adha na kero wanazozipata na ambazo zinahatarisha afya zao
Akizungumza kwa njia ya simu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida Bravo Liyapembile alisema ni kweli kuna changamoto katika machinjio yetu na tumeshachukua hatua ya kufanya marekebisho ya muda kwa kipindi hiki cha mvua ili kuweka vizuri hali ya upatikanji wa huduma ya nyama kwa walaji.
Kwasasa huduma ya uchinjaji inapatika katika machinjio ya mwakonko na kona ya mwamedi hivyo wananchi wasiwe na shaka katika upatikanaji wa nyama watendelea kupata huduma hiyo kama kawaida, wakati hatua za marekebisho kwa machinjio ya Kata ya Muhan’ga yakiendelea.
Katika hatua nyingine, Bravo amesema wameshapata eneo katika kijiji cha N’gaida eneo la Kisaki na tumeshafanya upembuzi yakinifu na hatua zote za awali ikiwemo michoro zimekwisha kamilika.
“Pale Kisaki kutakuwa na machinjio ya kisasa sanjari na kiwanda kikubwa cha kusindika ngozi, ambavyo thamani yake inakadiriwa kufikia zaidi ya shilingi bilioni tatu ambazo zitatolewa na Benki ya Dunia,” alisema Bravo.