Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Tathmini ya Utoaji wa Huduma za Afya ya Uzazi, Lishe na CHF iliyoboreshwa uliokutanisha wadau mbalimbali wa afya mkoani Shinyanga leo Alhamis Februari 27,2020 katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga. Picha zote na Kadama Malunde – Malunde 1 blog.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Tathmini ya Utoaji wa Huduma za Afya ya Uzazi, Lishe na CHF iliyoboreshwa uliokutanisha wadau mbalimbali wa afya mkoani Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Tathmini ya Utoaji wa Huduma za Afya ya Uzazi, Lishe na CHF iliyoboreshwa uliokutanisha wadau mbalimbali wa afya mkoani Shinyanga.
Wadau wa afya wakiwa ukumbini.
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Tathmini ya Utoaji wa Huduma za Afya ya Uzazi, Lishe na CHF iliyoboreshwa uliokutanisha wadau mbalimbali wa afya mkoani Shinyanga.
Afisa Lishe Mkoa wa Shinyanga, Dennis Madeleke akiwasilisha mada kuhusu hali ya Lishe mkoani Shinyanga.
Afisa Lishe Mkoa wa Shinyanga, Dennis Madeleke akiwasilisha mada kuhusu hali ya Lishe mkoani Shinyanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga Deborah Magiligimba akichangia hoja kwenye Mkutano wa Tathmini ya Utoaji wa Huduma za Afya ya Uzazi, Lishe na CHF iliyoboreshwa.
Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Kahama, Julius Chagama akichangia hoja ukumbini. Chagama alilalamikia kitendo cha wauza maziwa kuchanganya maji kwenye maziwa hali inayohatarisha afya za watumiaji.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Mhe. Nyabaganga Talaba akichangia hoja wakati wa mkutano huo.
Wadau wa afya wakiwa ukumbini.
Wadau wakiwa ukumbini.
Wadau wakiwa ukumbini.
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack ameziagiza halmashauri zote za wilaya mkoa wa Shinyanga na wadau wa afya kuongeza jitihada,mikakati na raslimali ili kutokomeza vifo vya uzazi na vifo vya watoto wachanga.
Telack ametoa agizo hilo leo Alhamis Februari 27,2020 wakati akifungua Mkutano wa Tathmini ya Utoaji wa Huduma za Afya ya Uzazi, Lishe na CHF iliyoboreshwa uliokutanisha wadau mbalimbali wa afya mkoani Shinyanga katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga.
Mkuu huyo wa mkoa alisema Takwimu zinaonesha kuwa kimkoa vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua na kufikia vifo 50 kutoka vifo 56 mwaka 2018 na vifo 73 mwaka 2017 hivyo kuzipongeza Halmashauri,hospitali na vituo vya vinavyotoa huduma za dharura za upasuaji kwa kuchangia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Alisema pamoja na takwimu za vifo vitokanavyo na uzazi kuonesha kupungua,bado kuna changamoto katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ambayo vifo viliongezeka kutoka vifo 5 mwaka 2018 hadi vifo 14 mwaka 2019.
“Hali hii inasikitisha,mara kwa mara nimekuwa naagiza kwamba viongozi na watendaji msimamie masuala ya uzazi. Katika mkoa huu sitaki kuona mama au mtoto mchanga anafariki wakati wa uzazi. Nawaagiza Halmashauri na na kuwaomba wadau wa afya tuongeze jitihada,mikakati na rasilimali ili kutokomeza vifo vya uzazi na watoto wachanga”,alisema Telack.
Katika hatua nyingine Telack alisema mkoa wa Shinyanga bado unakabiliwa na tatizo la lishe kwa watoto walio chini ya miaka mitano na akina mama walio kwenye umri wa kuzaa na kusisitiza kuwa kila mmoja anatakiwa kuwajibika kukabiliana na changamoto hiyo.
“Tatizo la upungufu wa damu kwa akina mama wenye umri wa kuzaa limepungua kutoka asilimia 59.4 mwaka 2015/2016 hadi asilimia 30.4 mwaka 2019. Kwa watoto walio chini ya miaka mitano udumavu umeongezeka kutoka asilimia 30% hadi asilimia 32.1%,ukondefu kutoka asilimia 2.4% hadi 4.3% wakati uzito pungufu kwa watoto umepungua kutoka 22% hadi 15%”,alieleza Telack.
Aidha alisema serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikichukua hatua za kukabiliana na utapiamlo mkoani Shinyanga ikiwemo kusaini mkataba wa utendaji wa masuala ya lishe kati ya mkuu wa mkoa,wakuu wa wilaya,wakurugenzi wa halmashauri,watendaji wa kata na vijiji ili kufuatilia viashiria vya lishe.
“Hatua hii imesaidia kuinua baadhi ya viashiria vilivyomo kwenye mkataba kwa mfano,akina mama wenye watoto wenye umri wa miezi 0 hadi miezi 23 wanapata elimu ya unasihi,watoto wanaendelea kupata matone ya Vitamin A, na matibabu ya utapiamlo yanaendelea kutolewa wenye vituo vya afya”,aliongeza Telack.
“Natoa wito kwa wadau wote wa afya ndani ya mkoa wetu kuendelea kushirikiana na serikali kutekeleza mipango mbalimbali iliyopo ili kuinua viashiria vyote vya lishe. Narudia tena kuziagiza halmashauri zote katika kipindi hiki cha maandalizi ya Mipango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/2021 zitenge shilingi 1,000 kwa kila mtoto aliye chini ya miaka mitano kwenye mapato ya ndani”,alisema.
Telack aliziagiza halmashauri kuweka mikakati ya kuongeza kiwango cha uandikishaji wa kaya katika Mfuko wa Afya ya Jamii ‘CHF iliyoboreshwa’ ili wananchi wafurahie huduma za kiafya kupitia CHF.
“Nawashukuru wadau wote kwa michango na misaada yenu mnayotoa katika kuboresha huduma za afya na lishe. Naomba muendelee kushirikiana na mkoa wetu ili tuweze kukabiliana na changamoto zinazotukabili katika utekelezaji wa afua za afya. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi na lishe”,alisema Telack.
Mkutano uliolenga kutathmini huduma za afya ya uzazi na mtoto,afua za lishe na uandikishaji wa kaya katika Mfumo wa Afya ya Jamii Ulioboreshwa (CHF iliyoboreshwa) umeenda sanjari na utoaji wa ngao na vyeti kwa halmashauri, hospitali na wadau waliochangia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi,kutekeleza mkataba wa lishe na kuinua kiwango cha kaya zilizoandikishwa kwenye CHF iliyoboreshwa.
Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt. Nuru Mpuya alizitaja halmashauri zilizopata ngao za Ushindi kutokana na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kuwa ni Kahama Mji,Kishapu na Ushetu.
“Halmashauri zilizopata ngao ya ushindi kutokana na kutekeleza vizuri mkataba wa lishe ni Ushetu,Kishapu na halmashauri ya Shinyanga. Kwa upande wa halmashauri zilizopata vyeti kwa ajili ya kutambua mchango wao katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ni Kahama Mji,Kishapu,Msalala,Shinyanga na Ushetu”,alifafanua Dkt. Mpuya.
“Halmashauri zilizopata vyeti kwa ajili ya kutambua mchango wao katika kuinua kiwango cha kaya kujiunga na CHF iliyoboreshwa ni Kahama Mji,Manispaa ya Shinyanga na Kishapu. Hospitali zilizopata vyeti kwa ajili ya kutambua mchango wao katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ni Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga,Hospitali ya wilaya ya Kahama,Hospitali ya Jakaya Kikwete Kishapu,Hospitali ya Mwadui na Kolandoto”,alisema.