Kaimu Makamu Mkuu wa chuo Prof. Ernest Kihanga akielekea kuzindua choo cha Wavulana Shule ya Msingi Mzumbe baada ya ukarabati.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mzumbe wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi, Walimu, Uongozi wa Kijiji na wawakilishi wa wanawake wa Jumuiya ya Chuo kikuu Mzumbe.
Kaimu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Kihanga (katikati) akiwa na Walimu, Viongozi wa shule, Wawakilishi wa Jumuiya ya Wanawake ya Chuo Kikuu Mzumbe na uongozi wa Kijiji.
Kaimu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.Kihanga akiteta jambo na Katibu wa kamati ya Wanawake wa Jumuiya ya Chuo kikuu Mzumbe Dkt.Saida Fundi. Wengine katika picha ni Bi. Rose Joseph, akifuatiwa na Mwenyekiti wa kamati Dkt. Eliza Lulu Genda na Bi.Juliana Kiombo Mjumbe wa Kamati wakiondoka eneo la tukio baada ya hafla ya makabidhiano.
Watoto wa Shule ya Msingi ya Mzumbe wakiwa na furaha baada ya makabidhiano ya jengo la Choo lililofanyiwa ukarabati kukamilika.
………………………………………………………………………………………………
Ikiwa zimebaki siku chache kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa Machi 8 kila mwaka, Jumuiya ya Wanawake ya Chuo Kikuu Mzumbe wakiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo wamekabidhi choo cha Wavulana kwa shule ya msingi Mzumbe baada ya kukifanyia ukarabati.
Akizungumza kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo wakati wa hafla ya makabidhiano, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Fedha na Utawala Prof. Ernest Kihanga, ameipongeza Jumuiya ya Wanawake wafanyakazi wa Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuendelea kuwa walezi wa Jamii kwani waliona hali mbaya ya choo hicho ilivyokuwa ikihatarisha afya za Wanafunzi na kupeleka ombi maalum kwa Uongozi wa Chuo kusaidia azma yao ya kuvikarabati.
“Kwa kutambua wajibu mkubwa tulio nao kama Taasisi ya Elimu ya Juu, lengo letu ni kuendelea kuhudumia shule zote zinazotuzunguka ili kuwa na mazingira bora ya kusoma, kwani wanafunzi hawa ndio wateja wa baadae wa Chuo chetu; hivyo ni muhimu wakaandaliwa mazingira bora ya kusomea ili kulinda afya zao na kuwa na ustawi mzuri wa kitaaluma” alisisitiza
Awali akisoma taarifa Mkuu wa shule hiyo Mwl. Philbert Songolo alisema kwa mara ya kwanza Jumuiya ya wanawake wa Chuo Kikuu Mzumbe ilitembelea shule hiyo mwaka 2017 na ndipo walibaini hali mbaya ya choo na kuamua kuendesha harambee ambayo iliwezesha mwaka 2018 kukarabati choo cha Wasichana.
Aliongeza kuwa baada ya ukarabati huo bado hali ya choo kwa upande wa Wavulana ilikuwa mbaya na hivyo ili kuleta usawa jumuiya hiyo ya wanawake waliamua kukarabati choo cha Wavulana, ukarabati ambao umegharimu jumla ya shilingi 1,103,400.00. Matokeo ya kazi hiyo yameongeza furaha, mahudhurio mazuri ya wanafunzi shuleni na kuwa chachu ya kuongeza ufaulu.
Pamoja na ukarabati huo kufanyika, bado shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa choo kulinganisha na Idadi ya wanafunzi ambapo kwa sasa idadi ya matundu ya choo ni 10 (kumi) kwa wastani wa tundu moja kutumiwa na zaidi ya wanafunzi 72, jambo ambalo si salama kwa afya za wanafunzi hasa linapokuja suala la milipuko ya magonjwa.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Shule Bw. Yusufu Ilomo akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Shule ameahidi kuendelea kufanyia kazi changamoto ya choo katika shule hiyo kwa kuwashirikisha kwa karibu wazazi ili kuendelea kulinda afya na mazingira ya watoto kusomea.