…………………………………………………………………………………………………..
Na Ahmed Mahmoud,Arusha
Vitendo vya ubakaji na kulawitiana kwa baadhi ya wanafunzi wa kiume wa shule za msingi jijini Arusha vimeelezwa kushamiri kiasi cha wanafunzi kushindwa kusoma,ambapo walimu wa shule hizo wameitaka jamii kuunganisha nguvu ili kutokomeza matukio hayo yanayosababishwa na utandawazi.
Hayo yamebainishwa jijini Arusha na baadhi ya walimu wa shule za msingi wakati wakipatiwa mafunzo maalumu juu ya vitendo vya ukatili na unyanyashaji dhidi ya wanawake na mtoto yaliyotolewa na shirika linalojihusisha na utetezi wa haki ya wanawake na watoto la cwcd la jijini hapa.
Mmoja ya walimu hao kutoka shule ya msingi Olasiti, Oliver Mbowe amesema kuwa pamoja na matukio ya ukatili kuwepo kwa baadhi ya familia ,vitendo vya kulawitiana kwa wanafunzi wa kiume vimeongezeka kiasi kwamba nguvu kubwa na ushirikiano kwa jamii inahitajika ili kutikomeza vitendo hivyo.
” Matukio mengi hivi sasa ni watoto kulawitiana tunachowaomba wazazi ,walezi na jamii kwa ujumla tushirikiane kufuatilia mienendo ya watoto wetu kwani haya matukio yanasababishwa na sisi wazazi kufanya ngono tukiwa na watoto wetu kwenye chumba kimoja cha kuishi” Amesema
Amebainisha kwamba katika shule ya Olasiti anayofanyiakazi matukio hayo yapo na watoto wengi wa kiume wanajihusisha na mchezo huo hasa wanapokuwa wanatoka shuleni ama wanatoroka wakati wa masomo.
Alisema kuwa utandawazi kwa mtoto kuangalia picha za ngono,pamoja na wazazi kushiriki tendo la ndoa katika chumba kimoja cha kuishi ni moja vyanzo vya mtoto kujifunza tabia hiyo mbaya.
Kufuatia kushamiri kwa vitendo hivyo shirika linalojihusisha na utetezi wa mtoto na wanawake la cwcd,limeamua kutoa semina kwa walimu ,viongozi wa dini na viongozi wa makundi mbalimbali kwa lengo la kuwaelimisha juu ya matukio ya ukatili na unyanyasaji .
Mkuu wa wilaya ya Arusha,Gabriel Dagarro amesema kuwa serikali ya wilaya kwa kushirikiana na vyombo vya dola imejipanga kuhakikisha matukio ya unyanyasaji,ubakaji ,ulawiti na ukatili hayaishii kwa kupatana bali wahusika wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Mkuu huyo amewataka wazazi na walimu kutoshiriki maelewano na watuhumiwa badala yake wawe mstari wa mbele kutoa taarifa polisi,ofisini kwake na ofisi zingine za serikali ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa na hatimaye kukomesha vitendo hivyo.