******************************
26. Februari 2020
Na Mwandishi Wetu
Watanzania wa leo nini kinawasibu kama wale wa enzi hizo ambao walidanganywa kwa vitu vidogo na kutoa vitu vyenye thamani kubwa kama vile almasi, dhahabu, pembe za ndovu na rasilimali watu kama watumwa kwenda
kuwafanyia kazi wengine na wao kukosa nguvu kazi hiyo.
Haiingii akilini dunia ya leo ambayo ni ya wasomi wanaojua mambo mengi ya dunia kuhadaika na kufanya shughuli au kazi zenye masilahi ya watu wengine
ambao wao wanakupatia ujira mkubwa bila kuwaza madhara ya ujira huo kwa Taifa lako.
Viongozi wetu wakuu wa kitaifa kwa nyakati tofauti na wakati wa ziara zao wamewahi kusema kuwa “Wakati umefika kwa watafiti wetu kuacha kuweka tafiti zao kwenye makabati na kuhakikisha zinafanyiwa kazi kwa manufaa ya Watanzania.
Nimekumbuka usemi huo ambao ni muhimu sana kwa watafiti wetu kuzingatia, lakini kuna agenda kubwa ambayo watafiti walio wengi wanafanya tafiti kulingana na agenda za bwana wakubwa. Ukifanya tafiti nje ya agenda
zao mara nyingi hupati ulichokusudia hata hivyo, unapokuwa na msimamo dhabiti kama mtafiti chochote unachokusudia kukifanyia utafiti utapata ufadhili.
Nchi isiyofanya utafiti ni kama imekufa, hivyo kufanya tafiti ni muhimu na ni lazima zilenge watu wa nchi husika kwa faida ya watu hao na sio vinginevyo.
Sasa inakuwaje unakubali kufanya tafiti ambazo hazina masilahi na nchi yako unafanya kwa faida ya nani? Na ni nani anayekushawishi kuwadhuru hata watu wako kwa faida ya watu wengine watoka mbali.
Kwa nini usijivunie na kujiuliza nimeifanyia nini Tanzania katika maisha yangu yote ambayo Mungu amenipa hapa duniani kwa manufaa ya Taifa langu, badala ya kukumbukwa kwa kuwaneemesha watu wasioridhika walionyonya binadamu wenzao tangu enzi hizo za ujima kwa kusomba rasilimali zetu na nguvu kazi lakini hadi leo wanapambana kusimika utaratibu huo katika bara la
Afrika?.
Katika simulizi za huko nyuma tuliambiwa babu zetu walidanganywa na wakoloni ambao wengine walikuja kutafuta rasilimali zetu na kuwaletea babu zetu shanga, nguo na wao babu zetu wakawapa almasi, dhahabu, pembe za ndovu na rasilimali watu wa kwenda kuwatumikia katika nchi zao. Viongozi hao hawakufahamu na kutambua kuwa walikuwa wanauza utu wa watu wao na hawakujua kama mawe wanayowapa ni rasilimali muhimu kwa uchumi wa himaya zao walizokuwa nao enzi zile.
Jiulize leo hii Watanzania hawajui wanaokuja kwetu wanataka nini?
Anayekutuma au kufanya nae kazi anataka nini na Taifa lako linataka nini kwake ? Tunaweza kurudia makosa waliofanya babu zetu na kuuza utu wetu kwa minajili ya kulipwa ujira mkubwa?