Home Mchanganyiko WANANCHI WA MAKONGOLOSI CHUNYA WALILIA BARABARA

WANANCHI WA MAKONGOLOSI CHUNYA WALILIA BARABARA

0

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, akitoa maelekezo kwa wahandisi wanaosimamia mradi wa ujenzi wa barabara ya Chunya- Makongolosi (Km 39) kutoka kampuni ya SMEC alipokuwa akikagua daraja la mto Lupa, mkoani Mbeya.

Mhandisi Mshauri kutoka Kampuni ya SMEC, Daniel Goshima, akimuonesha Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga (Wanne kulia), nguzo za daraja jipya la mto Lupa (halipo pichani), ambalo linajengwa pembezoni mwa daraja la zamani, mkoani Mbeya.

Muonekano wa nguzo za daraja jipya la mto Lupa ambalo linajengwa na Mkandarasi China Railway 15 Bureau Group Corporation. Ujenzi wa daraja hilo ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Chunya – Makongolosi (Km 39), mkoani Mbeya.

Wafanyakazi wa Mkandarasi China Railway 15 Bureau Group Corporation, anayejenga barabara ya Chunya- Makongolosi (Km 39) wakiendelea na kazi za ujazaji wa mawe na kifusi katika daraja la Chipoka, mkoani Mbeya.

Muonekano wa barabara ya Chunya – Makongolosi (Km 39) kwa kiwango cha lami ambapo ujenzi wake unaendelea. Mradi huu umefikia asilimia 61 na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai mwaka huu.

PICHA NA WUUM

………………………………………………………………………………………………………….

 Wananchi  wa Makongolosi Wilayani  Chunya, mkoani Mbeya, wameiomba Serikali kuharakisha  ujenzi  wa barabara ya Chunya – Makongolosi (Km 39), kwa kiwango cha lami  ili kutataua changamoto ya usafiri na usafirishaji katika eneo hilo.


Akizungumza wilayani Chunya, mkoani Mbeya, mmoja wa wananchi hao, Joana Makwezo, amesema kuwa kujengwa kwa barabara hiyo kwa kiwango hicho kutarahisisha huduma za usafirishaji na kutasaidia kukuza shughuli za kijamii na kiuchumi ikiwemo biashara ya madini ambayo ndio biashara kuu katika eneo hilo.


“Tunaiomba Serikali itusaidie barabara hii ikamilike haraka, sisi wengine ni wagonjwa  na tunachelewa kwenda kupata huduma za matibabu kutokana na changamoto ya barabara, wakati mwingine huduma za usafiri zinakuwa juu kutokana na changamoto ya barabara na umbali, naamini barabara ikikamilika hata vyombo vya usafiri vitaongezeka na gharama za usafiri zitashuka”, amesema Joana Makwezo


Naye, Dereva Ally Kondo, amesema kuwa wasafirishaji wengi wanashindwa kuleta magari katika eneo hilo kutokana na kuwepo kwa changamoto katika barabara hiyo, hivyo anaamini kuwa ujenzi kwa kiwango cha lami pindi utakapokamilika, utapelekea magari mengi kuongezeka na wasafiri kufika kwa wakati katika shughuli zao.

Ameiomba Serikali kuziba mashimo yaliyopo kwenye njia mbadala inayotumika sasa   kwani magari mengi huharibika kutokana na kuwepo kwa mashimo kwenye barabara hiyo.

 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, amesema kuwa mradi huo unaendelea vizuri na hivyo kumtaka Mkandarasi kuongeza kazi ya ujenzi ili barabara hiyo ikamilike haraka kwa viwango na kwa muda uliopangwa. 

Mwakalinga, amempongeza Mkandarasi huyo kwa kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga kituo cha Afya ambapo amemuelekeza mkandarasi huyo kutatua changamoto za kitaalamu alizozibaini katika mradi huo kabla ya kukabidhi kwa Serikali.

Ametoa wito kwa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kuhakikisha wanatoa maelekezo na kuweka vibao vya kiusalama katika maeneo ambayo yanajengwa barabara hususan katika vipindi hivi vya mvua ili kumsaidia dereva kutambua njia sahihi ya kupita. 

Aidha, amemtaka Mkandarasi anayejenga barabara hiyo kukarabati njia mbadala inayotumiwa na wasafirishaji ili kuondoa changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo kuwepo kwa mashimo katika baadhi ya maeneo.

Awali wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi kwa Katibu Mkuu huyo,  Mhandisi Mshauri, Daniel Goshima, amemuhakikishia Mwakalinga kumaliza mradi huo kwa wakati na kwamba kwa sasa umefikia asilimia 61 na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai mwaka huu.

Mradi wa ujenzi wa barabara ya Chunya- Makongolosi (Km39) ni seehemu ya barabara iliyo katika ushoroba wa kati magharibi, yaani Mbeya- Rungwe- Ipole – Tabora hadi Nzega na inafadhiliwa na Serikali kwa asilimia mia moja.