Home Mchanganyiko WAATUMISHI MIZANI WAASWA KUJIEPUSHA NA RUSHWA

WAATUMISHI MIZANI WAASWA KUJIEPUSHA NA RUSHWA

0

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, akimuelekeza jambo Mhandisi Mshauri wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Sumbawanga- Matai- Kasanga Port (Km 117), kwa kiwango cha lami, mkoani Rukwa.

Muonekano wa daraja la mto Kalambo lililopo kwenye barabara ya Sumbawanga- Matai- Kasanga Port (Km 117). Daraja hili lina urefu wa mita 40 na utekelezaji wa ujenzi wake umefikia asilimia 100

Muonekano wa barabara ya Sumbawanga- Matai- Kasanga Port (Km 117), kwa kiwango cha lami. Barabara hii imefikia asilimia 94.6 na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka huu.

Muonekano wa mizani ya Matai, mkoani Rukwa. Utekelezaji wa ujenzi wa mizani hii umefikia asilimia 99.

PICHA NA WUUM

**************************

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, amewataka watumishi wa mizani kuzingatia Kanuni na Sheria za Utumishi na kuepuka kujihusisha na vitendo vya rushwa.

 

Hayo ameyasema wakati wa ukaguzi wa barabara ya Sumbawanga- Matai- Kasanga Port yenye urefu wa Km 117 ambayo inajumuisha mradi wa mizani ya Matai na daraja la mto Kalambo lenye urefu wa mita 40.

 

Ameeleza kuwa Serikali inatumia fedha nyingi katika utekelezaji wa Miundombinu hususani ujenzi wa barabara, hivyo vitendo vya kukubali kupokea rushwa kwenye magari yaliyozidisha uzito ni kosa kubwa la uhujumu uchumi.

 

“Hakikisheni mnafanya kazi kwa uadilifu kwani Wizara imeanza utaratibu wa kufuatilia utendaji kazi wa watumishi wa mizani masaa 24 kwa kutumia mfumo wa kamera na tayari watumishi 15 wamekamatwa na wanahojiwa na Jeshi la Polisi”, amesema Mwakalinga.

 

Akiwa katika daraja la Mto Kalambo, Katibu Mkuu amempongeza Mkandarasi wa mradi huo kwa kujenga daraja lenye ubora na kumsisitiza kumalizia kipande cha barabara hiyo ambacho hakijakamilika kwa muda
uliobakia.

 

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri wa mradi huo kutoka kampuni ya Nicholas O' Dweyer, Martin Hurssey, amesema kuwa mradi umefika asilimia 94.6 na kazi zilizokamilishwa ni pamoja na ujenzi wa barabara hiyo
hadi kufikia  km 106.2 kwa sasa, ujenzi wa mizani, daraja na round about.

 

Ameongeza kuwa ujenzi wa mizani ulihusisha ujenzi wa ofisi, eneo la kupimia uzito wa magari, njia za zege za kuingilia na kutokea katika eneo la mizani pamoja na eneo la maegesho lililojengwa kwa kiwango cha zege.

“Mzani huu umekusudiwa kuhudumia barabara mbili yaani Sumbawanga- Matai- Kasanga Port na Matai – Kasesya na kwa sasa ujenzi wake, umefikia asilimia 99″, amesema Hurssey.

 

Mradi wa ujenzi wa barabara ya Sumbawanga- Matai- Kasanga Port (Km 112), ni moja ya mradi ambao umefadhiliwa na Serikali kwa asilimia 100.

 

Mradi huu umefikia asilimia 94.6 mpaka sasa ambapo umegharimu Bil 133 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka huu.