Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro, Ndaki Mhuli akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Godson Ngomuo na Makamu Mwenyekiti Juma Juni.
*********************
HALMASHAURI ya Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro, imetumia sh69 bilioni kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia mapato ya halmashauri, fedha za ruzuku za serikali kuu, michango ya wananchi na wadau wa maendeleo.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Siha, Ndaki Mhuli alisema wamefanikisha miradi hiyo kwa lengo la kuwanufaisha wananchi wa eneo hilo.
Mhuli alisema hivi karibuni wametumia sh248 milioni kwa ajili ya mikopo ya vikundi vya wanawake 1,790 na sh79 milioni kwa ajili ya vikundi 24 vya vijana na sh14 milioni kwa vikundi vitatu vya watu 34 wenye ulemavu.
“Mikopo hiyo imewawezesha vijana, watu wenye ulemavu na wanawake wa halmashauri ya wilaya ya Hai, kuanzisha miradi ya kiuchumi ya ufugaji, kilimo, uvuvi, usindikaji mazao na biashara katika sehemu mbalimbali,” alisema Mhuli.
Alisema wanaishukuru serikali ya awamu ya tano ya Rais John Pombe Magufuli kwa kufanikisha kuwapatia sh1.5 bilioni za ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya ambayo inaendelea kujengwa hadi hivi sasa.
Alisema wamefanyia matengenezo kilomita 113.6 ya mtandao wa barabara za wilaya ya Siha kwa kutumia sh555 milioni, kufanya matengenezo sehemu korofi kilomita 95.16 kwa sh823.4 milioni na kilomita 43.85 za matengenezo ya muda maalum kwa sh812.7 milioni.
Alisema walitumia sh165 milioni kwa ajili ya kujenga skimu ya umwagiliaji kwenye kijiji cha Kishisha na wakafanikisha mafunzo kwa wakulima ili waweze kuchangia katika uendeshaji wa skimu yao.
Alisema serikali imefanikisha miradi ya maji ya thamani ya sh3.135 bilioni na hivi sasa wanatekeleza miradi miwili ya maji kwenye vijiji vya Makiwaru na Magadini na mradi wa Lawate Fuka.
Alisema kupitia wakala wa umeme vijijini (Rea) wamefanikiwa kufikisha nishati ya umeme kwenye vijiji 57 kati ya vijiji 60 huku vitongoji 127 kati ya vitongoji 169 vikiwa vimepata wanapambana katika vijiji vitatu na vitongoji 42 vilivyobaki.
Alisema zaidi ya ajira mpya 537 zimepatikana zikiwa za moja kwa moja kutoka kwenye makampuni na mashamba makubwa mbalimbali yaliyopo kwenye eneo hilo la halmashauri ya wilaya ya Siha.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Siha, Godson Ngomuo aliwapongeza madiwani, wataalamu wa serikali na wananchi kwa ujumla katika kufanikisha hayo.
“Tunatarajia mazuri zaidi yatafanyika hapa kwetu Siha hasa tukitambua kuwa huu mwaka ni kipindi cha mshikemshike kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani,” alisema Ngomuo.