Klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam imeweka rekodi mpya tangu miaka 10 iliyopita kwa kutoka sare mechi nne bila kupata ushindi na kwa matokeo hayo rasmi imejiondoa katika kinyang’anyiro cha kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Vodacom Tanzania bara.
Yanga wamecheza mechi ya nne jijini Tanga na kulazimishwa sare ya bila kufungana na wenyeji Coastal Union mchezo uliomalizika kwenye uwanja wa Mkwakwani hii ni sare ya pili wakiwa ugenini na mbili wamepata wakiwa uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo, Yanga inaendelea kushika nafasi ya nne wakiwa na Pointi 41 huku Namungo wakishika nafasi ya tatu kwa pointi zao 43 hata hivyo Yanga wanamchezo mmoja mkononi.
Kwa Matokeo hayo Yanga wanazidiwa Pointi 21 na Simba wenye pointi 62 waliocheza mechi 24 huku Yanga akicheza mechi 22 licha ya kufungwa jana Azam FC bado wapo nafasi ya pili kwa Pointi 45.
Shujaa wa Yanga leo ni Mlinda mlango wao Metacha Mnata ambaye ameweza kuokoa michomo mikali kipindi cha pili kutoka kwa washambuliaji wa Coastal Union wakiongozwa na Ayoub Lyanga .
Ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara itasimama katika mwa wiki ya kesho kupisha michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam Fc ambapo Jumanne mabingwa Simba watakuwa mjini Shinyanga kucheza na Stand United huku Yanga wakicheza na Matajiri wa daraja la kwanza kutoka Misungwi timu ya Gwambina FC uwanja wa Taifa Dar es Salaam Siku ya Jumatano.