…………………………………………………………………………………………….
NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO
MKUU Wa Wilaya Ya Bagamoyo ,Zainab Kawawa ameiagiza halmashauri ya Bagamoyo kutumikia wananchi kwa maslahi mapana ya jamii pamoja na kusimamia chanzo kikuu cha machimbo ya mchanga ambacho kinalegalega na kusababisha kushuka kwa mapato.
Aidha mkuu huyo wa wilaya, ameelekeza kupatiwa maelezo ya kina ni kwanini mashine za makusanyo (posi) zinazimwa na kushindwa kukusanya mapato kwa muda mrefu na hivyo kuhitaji maelezo ofisini kwake.
Akizungumza na watumishi na madiwani wa halmashauri hiyo, Zainab alisema , wabadilike ,wasimamie na kufuatilia mapato pasipo kujenga uongo na udanganyifu kwa maslahi ya matumbo yao.
“Haiwezekani mapato ya mchanga yanashuka ,licha ya vyombo vya ulinzi na usalama kubaini mianya na udanganyifu, hasa katika eneo hili la mchanga, mmefikia hatua ya kuidanganya hadi TAKUKURU mnapotosha taarifa na takwimu sahihi za makusanyo ili kujinufaisha””
“Ninahitaji maelezo pia kwanini mnazima posi ,hizi mashine mnazima kwa kipi?!nahitaji maelezo na nakala nyingine ielekezwe kwa mkuu wa mkoa na nyingine TAMISEMI”alisema Zainab.
Zainab alieleza, kuzimwa kwa posi ni kukiukwa maelekezo ya TAMISEMI ,halmashauri ni eneo lenye heshima na hadhi yake,ambapo inapaswa kuendeshwa kwa kuzingatia sheria,kanuni na taratibu hivyo pasifanyiwe mchezo ama kuendeshwa kiholela (kihuni).
Nae mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ally Ally Issa alisema , hali ya mapato hairidhishi kutokana na chanzo mama cha mchanga kuyumba ambapo makusanyo yamefikia asilimia 43 wakati walitakiwa kufikia asilimia 50 kwa kipindi hiki cha miezi sita.
Alifafanua kwamba, kutokana na hilo wamebaini machimbo holela ya mchanga 23 na sasa wapo katika mkakati wa kuyafunga baadhi ya machimbo na mengine kuyarasimisha na kuongeza usimamizi ili kunusuru utoroshaji na kuongeza mapato.
Alieleza kwamba, machimbo ambayo yamesharasimishwa ni pamoja na Nzole,Fukayose na Mapinga.
Kuhusu posi ,Ally alieleza tatizo kubwa kuna nyingine zimeharibika na nyingine hazifanyikazi hivyo pia wamenunua posi mpya 43 ili kupunguza changamoto iliyojitokeza.
Kwa upande wake ofisa mazingira Bagamoyo, Cleophace Murugwa aliwataka wachimbaji kufuata taratibu za kupata kibali na leseni .
Alibainisha ,kwasasa wanapambana na wale wanaofanya uchimbaji wa maeneo yasio rasmi, na atakaeenda kinyume na taratibu sheria inachukua nafasi yake.
Murugwa alitaja maeneo yaliyo rasmi ni Kilomo eneo la Buma, Yombo -Chasimba na Fukayose huko Mwavi.