**************************
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesaini makubaliano ya ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Plan International, kutoa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana 400 mkoani Mwanza kupitia mradi wa Vijana na Ubunifu katika Kazi (VUKA).
Akizungumza wakati wa tukio la utiaji saini makubaliano hayo leo tarehe 21 Februari, 2020 katika ofisi za VETA Makao Makuu Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkazi wa Plan International Tanzania Dkt. Mona Girgis amesema kuwa makubaliano hayo yanalenga hasa kutoa mafunzo ya ufundi stadi yatayowezesha vijana wanaotoka katika mazingira magumu mkoani Mwanza kupata ujuzi utakaowawezesha kujipatia ajira.
Dkt. Girgis amesema kuwa mradi wa VUKA utatekelezwa katika Wilaya za Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza na utamalizika mwaka 2021 ukifadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya (EU) na shirika la Plan International la nchini Ubelgiji.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu amesema kuwa VETA imekuwa ikishirikiana na Plan International katika kutekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kutatua changamoto ya ajira kwa vijana na hivyo kuwekwa rasmi kwa ushirikiano huo ni jambo muhimu.
Dkt. Bujulu amesema kuwa VETA kupitia chuo cha VETA Mwanza itakuwa na jukumu la kudahili na kutoa mafunzo kwa vijana wanaotoka kwenye mazingira magumu, kutoa
ushauri wa kitaaluma na kuwaunganisha vijana na fursa mbalimbali ikiwemo makongamano ya vijana.
Mdhibiti wa Fedha kutoka shirika la Plan International la nchini Ubelgiji, Sibylle Gilbert amesema shirika lake linaona fahari kufadhili mradi huo na anaamini kuwa ushirikiano kati ya VETA na Plan International utaleta manufaa makubwa kwa vijana hapa nchini.