Home Makala MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO KATIKA SEKTA YA MAENDELEO YA...

MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO KATIKA SEKTA YA MAENDELEO YA JAMII

0

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu katika akishiriki ujenzi wa vyumba vya bweni la Wasichana shule ya Sekondari Kirare Jijini Tanga ikiwa ni kuunga mkono juhudi za wananchi kushoto ni Diwani wa Kata hiyo (CCM) Mwagilo anayefurahia ni Mkuu wa wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Faustine Ndugulile akishiriki kutengeneza tofali na wananchi wa Kata ya Chambasi katika ujenzi wa shule ya msingi Chambasi Wilayani Kisarawe.

Wananchi wa Kijii cha Chibumagwa pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu mwenye miwani wakibeba tofali wakati wa Kampeni ya Kitaifa kuhamasisha wananchi kuboresha makazi inayoendelea katika vijiji mbalimbali nchini ikiwa imenaza na vijiji vilivyopo katika Kata ya Sasajila Wilayani Manyoni. 

Picha na Wizara.

……………………………………………………………………………………………………………..

Na.Alex Sonna,Dodoma

KATIKA kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya tano, Sekta ya Maendeleo ya Jamii nchini  ni miongoni mwa sekta zilizopata mafanikio mbalimbali katika kuhakikisha jamii inajileletea maendeleo kwa kutumia fursa zilizopo.

Jukumu hilo limetekelezwa kwa kushirikisha, kuhamasisha, kuelimisha na kuwezesha jamii kuzingatia umuhimu wa maendeleo ya jinsia, wazee na watoto.

Makala hii inaelezea mafanikio manne yaliyopatikana ndani ya kipindi hicho katika Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto ambayo ipo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mafanikio hayo ni pamoja na uwezeshaji wanawake kiuchumi, Huduma kwa wazee, Ustawi wa watoto na usimamizi wa mashirika yasiyo ya kiserikali.

Idara hiyo pamoja na mambo mengine inashughulikia masuala ya ustawi na jinsia kwa kuweka kipaumbele katika kuwezesha wanawake kiuchumi.

UWEZESHAJI WANAWAKE KIUCHUMI

Katika jitihada za Wizara kuwezesha wanawake kiuchumi Serikali kupitia Benki ya Posta Tanzania imeendelea kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.

Kiasi  cha Sh.Bilioni 2.5 zimetolewa kwa wanawake wajasiriamali 3,035 kutoka katika mikoa 26 ya Tanzania

Bara.

Pamoja na utoaji mikopo yenye masharti nafuu Serikali pia imeendelea kuhamasisha wanawake kujiunga na SACCOS na VICOBA ambapo jumla ya SACCOS 130 za

wanawake zilianzishwa katika mikoa ya Mara, Mwanza, Tanga, Kigoma, Dodoma, Kagera, Shinyanga, Simiyu, Rukwa, Ruvuma, Mbeya, Lindi, Mtwara, Geita, Manyara na Dar es Salaam.

Hata hivyo, Serikali imekuwa ikitoa Mafunzo

kuhusu urasimishaji na uboreshaji wa bidhaa na kuunganishwa na Mamlaka za Udhibiti

wa Ubora wa Bidhaa (TFDA, TBS na SIDO) yalitolewa kwa wanawake wajasiriamali 7,713 ili kuongeza ubora wa bidhaa na kuwawezesha kupata taarifa za masoko ya

bidhaa zao.

Pamoja na utoaji mafunzo ya ujasiliamali kwa Wanawake, Serikali pia imeendelea

kutenga fedha asilimia 5 ambayo sasa imekua asilimia 4 kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake katika Halmashauri 185.

Aidha, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya Mfuko huo unaongezeka kila Mwaka ambapo mwaka 2015/16, Sh.Bilioni 3.4 zilitolewa, mwaka 2016/17, Sh.Bilioni 8.8 mwaka 2017/18, Sh.Bilioni 16.3 na mwaka

2018/19, Sh.Bilioni 11.1 zilitolewa ili kuwezesha wanawake wengi zaidi kuinuka kiuchumi.

Katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Mkoa wa Rukwa mwaka 2018, Waziri wa wizara hiyo, Ummy  Mwalimu, anawataka Wakurugenzi wa Halmashuri zote nchini kutenga asimilia 4 kwa ajili ya wanawake na

kutoa mikopo yenye tija itakayoweza kuwasaidia wanawake kuongeza vipato vyao ili kujikwamua kiuchumi.

Waziri Ummy anasisitiza kuwa ili kufikia azma ya Tanzania ya Viwanda Halmashauri hazina budi kujiwekea mikakati ya kutoa mikopo mikubwa itakayo wawezesha wanawake na wananchi kwa ujumla kufikia azma hiyo.

Kuhusu utekelezaji wa agizo hilo kutoka kwa Waziri, Halmashauri 185 zimetoa Sh.Bilioni 39.7 katika Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake kwa kipindi cha miaka minne ili kuwezesha mikopo yenye masharti nafuu kwa wanawake

wajasiriamali 877,071.

Aidha, Serikali imefanya uhamasishaji kwa wanawake kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii na kutoa mafunzo kwa wanawake wajasiriamali 207 mkoani Mwanza kuhusu kujiunga na mifuko ya NSSF na NHIF.

Pamoja na Serikali kuhamasisha wanawake kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii pia imefanya marekebisho ya Sheria ya Fedha Na. 4 ya mwaka 2018 na kurekebisha

Sheria ya Fedha za Mamlaka za Serikali za Mitaa Sura ya 290 kwa kuongeza Kifungu kipya cha 37A ambacho kinaelekeza Halmashauri zote kuchangia asilimia 10 ya

mapato yao ya ndani ili kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Serikali imeweka utaratibu wa kuondoa kero kwa wajasiriamali wanawake ambapo Mamlaka za Serikali za Mitaa zinawajibika kutenga maeneo ya kufanyia biashara kwa wajasiriamali wakiwemo wanawake na sasa Halmashauri 150 zimetenga maeneo ya shughuli za biashara na viwanda.

Serikali imetenga maeneo rasmi yenye ukubwa wa hekta 15,822.64 kwa ajili ya kufanyia biashara kwa wajasiriamali wakiwemo mama lishe na wauza mbogamboga katika mikoa ya Arusha, Iringa, Mara, Rukwa, Tanga, Shinyanga, Mwanza, Kilimanjaro,

Singida, Morogoro, Singida, Manyara, Njombe, Kagera, Dar es Salaam, Dodoma, Lindi, Geita, Tabora na Ruvuma.

HUDUMA ZA WAZEE

Idara hiyo imekuwa na jukumu la kushughulikia ustawi wa wazee nchini na imendelea kuhakikisha wazee wanatambuliwa na kupatiwa huduma za matibabu bila malipo.

Akizungumza katika Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee Duniani hivi karibuni Mkoani Mtwara Waziri Ummy, anasema Serikali imewatambua wazee 1,897,021 katika Halmashauri 185 kwenye mikoa 26 ya Tanzania Bara ambapo wazee 766,227 wamepatiwa vitambulisho vya matibabu sawa na asilimia

40.                  

Aidha Waziri Ummy anaongeza kuwa Wazee waliopatiwa vitambulisho vya matibabu bure wameongezeka kutoka wazee 213,025 akiwataja wanaume kuwa 106,129 na wanawake 106,896 mwaka 2015/16 hadi kufikia wazee 766,227 ambapo wanaume ni 391,647 na wanawake ni 374,577 kufikia mwezi Juni, 2019.

Naye, Katibu Mkuu anayeshughulikia Idara hiyo,

Dk. John Jingu, anasema Serikali inatoa huduma za msingi za chakula, malazi, mavazi na matibabu kwa wazee wasiojiweza wanaoishi katika makazi 16 ya wazee yanayomilikiwa na Serikali.

Dk. Jingu pia anasema Mkakati wa Kutokomeza Mauaji ya Wazee (2018 – 2023) umeandaliwa ili kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu haki za msingi kwa wazee na

kuongeza kuwa kuna Mabaraza ya wazee 8,183 yameanzishwa katika Halmashauri ili kuwezesha upatikanaji haki kwa wazee nchini.

USTAWI WA WATOTO

Dk.Jingu anasema ili Kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya uonevu, ukatili, udhalilishaji, Utumikishwaji

na mila potofu Serikali imeanzisha Mtandao wa Mawasiliano ya Simu Na. 116

umeanzishwa ili kuwezesha jamii kutoa taarifa za vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.

Kupitia mtandao huu, jumla ya watoto 3,833 waliofanyiwa vitendo vya ukatili waliwezeshwa kupata huduma za chakula, vifaa vya shule, huduma za sheria na afya.

Aidha, Serikali imeanzisha vituo vya huduma za pamoja kushughulikia wahanga wa ukatili 13 katika Mikoa 9 ya Tanzania Bara ambayo ni Mbeya, Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro, Arusha Shinyanga, Iringa, Mwanza na Tabora. Vituo hivi hutoa huduma jumuishi kwa

wahanga wa ukatili hususan kwa wanawake na watoto.

Kadhalika, Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto 11,520 zimeanzishwa ambapo kamati 2 zimeanzishwa katika ngazi ya Taifa, 26 ngazi ya Mkoa, 112 ngazi ya Halmashauri, 2,592 ngazi ya Kata, na 8,788 ngazi ya Kijiji/Mtaa.

Pi anasema serikali imeratibu upatikanaji wa huduma za misingi za malazi, chakula, mavazi, matibabu na elimu kwa watoto walio katika mazingira hatarishi wanaoishi katika makao ya watoto katika mikoa 26.

“Watoto wanaoishi katika makao ya watoto wanaongezeka kila mwaka ambapo mwaka 2015/16 makao ya watoto yalihudumia watoto 4,379, mwaka 2016/17, watoto 4,515; mwaka 2017/18, watoto 6,132; na mwaka 2018/19, watoto 13,420,”anasema

Katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Afrika mwaka huu Mkoani Geita, Waziri Ummy anasema katika kuimarisha haki ya ushiriki wa mtoto, Serikali kwa

kushirikiana na wadau imeendelea kuhimiza Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuongeza bajeti ya kuwezesha utendaji wa mabaraza ya watoto.

Anasema mabaraza hayo yanatoa fursa kwa watoto kujadili masuala mbalimbali yanayohusu haki na ustawi wao na pia kuishauri Serikali kuhusu masuala hayo.

Vilevile, Waziri Ummy anaongeza kuwa mpaka kufikia mwezi Machi, 2019 Serikali ilianzisha mabaraza ya watoto 19 katika ngazi ya mikoa, mabaraza 121 katika ngazi ya Halmashauri za Manispaa, Wilaya, Miji, mabaraza 733 katika ngazi ya Kata na mabaraza 795 katika ngazi ya kijiji ambayo yamekuwa na mchango

Mkubwa.

Katika kuimarisha ustawi na maendeleo ya familia nchini, Wizara imetoa mafunzo ya malezi chanya kwa wazazi na walezi 635 kwenye ngazi ya familia kwenye Halmashauri

132 katika mikoa 26 chini kuhusu stadi za malezi chanya kwa watoto.

Aidha, elimu hiyo imewezesha kuanzishwa kwa vikundi vya Malezi 1,184 katika Halmashauri 15 katika

mikoa 7.

 

USIMAMIZI WA MASHIRIKA

YASIYO YA KISERIKALI

Kwa kipindi hicho, serikali imeendelea kusajili, kufuatilia na kuratibu shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali

nchini ili kukuza mchango wa mashirika hayo katika kusaidia jamii kufikia maendeleo yao.

Serikali imeanzisha Mfumo wa kielectroniki wa uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) unaowezesha kufanyika kwa malipo ya ada mbalimbali

inayotekelezwa na NGOs na wanufaika wa miradi.

Aidha anasema mfumo huu unasaidia kujua kiasi cha fedha kilichotumika pamoja na wafadhili wa fedha kwa miradi inayotekelezwa ili kujenga uwazi na uwajibikaji ikiwa ni pamoja na kuboresha uratibu wa mashirik kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya Taifa.