Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi katikati mwenye miwani akiwa na baadhi ya washiriki wa Kongamano la Wanawake Kanda ya Kati, lililofanyika Singida juzi.
Baadhi ya washiriki kutoka mikoa ya Tabora, Dodoma na Singida wakisikiliza mada mbalimbali kwenye Kongamano la Wanawake Kanda ya Kati, lililofanyika mkoa wa Singida.
Kongamano la Wanawake likiendelea.
Wanawake wakiwa kwenye kongamano hilo.
Wakina baba wakijumuika kwenye kongamano hilo.
Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Singida, Jonathan Semiti akiwasilisha mada katika kongamano hilo.
Mshiriki wa Kongamano hilo Stela Mwenigoha kutoka Faraja Centre akichangia.
Na Godwin Myovela, Singida
WAKIWASILISHA hali halisi ya takwimu za vitendo vya ukatili wa kijinsia nchini kwa kati ya mwaka 2016/18, Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, John Mapunda na Juliana Ntukey kwa nyakati tofauti, kupitia Kongamano la Wanawake kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani mkoani hapa jana, walisema vitendo hivyo vinazidi kuongezeka
2016 idadi ya matukio ukatili wa kijinsia na unyanyasaji yaliyoripotiwa yalikuwa 31,996 na ilipofika 2018 yaliongezeka na kufikia 43,487 huku mikoa 6 iliyoonyesha kukithiri kwa matukio hayo ikiwa Dar es Salaam, Morogoro, Singida, Dodoma, Tanga na Arusha
Kwa mujibu wa takwimu 2016 Temeke (4, 101), Morogoro (3,073), Singida (2,567), Arusha (2,890) na Tanga (1,904), huku mwaka uliofuata 2017 Kinondoni iliongoza kwa matukio (7,854), Dodoma (3,927), Temeke (3,163), Singida (2,890) na Arusha (2,790)
Mwaka 2018 mkoa ulioongoza kwa matukio ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji ulikuwa Kinondoni (5,386), Temeke (3,999), Arusha (3, 904), Tanga (3,252), Dodoma (1,882).
Huku idadi ya watoto waliofanyiwa ukatili wa kijinsia katika kipindi hicho ikiongezeka kutoka (10, 551) mwaka 2016 hadi kufikia (14, 491) mwaka 2018. Takwimu zinaonyesha idadi hasa ya watoto wa kike ni kubwa na imekuwa ikiongezeka mwaka hata mwaka, ilinganishwa na wale wa kiume
“2016 watoto wa kike walioripotiwa kufanyiwa ukatili walikuwa 8, 496 huku wa kiume wakiwa 2, 055, mwaka 2017 wakike walikuwa 9,810 wakiume wakiwa 3647, na mwaka 2018 watoto wa kike walikuwa 11, 789 huku wa kiume wakiwa 2, 702,” anasema Mapunda.
Baada ya takwimu hizo kuwasilishwa wanawake walipata fursa ya kuchangia, ambapo pamoja na mambo mengine, imeshauriwa kuanzishwa kwa vikundi huru vya wanafunzi kwenye maeneo ya shule ambavyo vitasimamiwa na walimu wa shule husika (clubs).
Lengo la vikundi inaelezwa kuwa itakuwa ni kupeana elimu na kuhamasishana juu ya masuala yote yanayohusu ukatili na hatua zinazopaswa kuchukuliwa punde tu tukio hilo linapojitokeza miongoni mwa mtoto yeyote
Kupitia Kongamano hili linalofadhiliwa na Mfuko wa Ruzuku kwa Msaada wa Kisheria (LSF) chini ya uratibu wa shirika la SEMA lenye makao yake makuu mkoani hapa, imebainika wazi kwamba watoto wengi kwa sasa wameonekana kubakwa na wengine kulawitiwa kwa siri wakiwa majumbani na mashuleni, na hutishiwa na wahalifu kwamba wasiripoti popote
Watoto wanaendelea kukaa kimya wakiteseka ndani kwa ndani kwa maumivu makali-hatimaye inapita mda mrefu-hana wa kumweleza, mzazi yupo ‘bize’ na shughuli za maisha, hana hata mda wa kumsikiliza mtoto
“Kwa kukosa uhuru na wazazi wao wa kuwaeleza matatizo yanayowapata wahanga wengi wamegundulika kuwa wamebakwa na kulawitiwa baada ya mda mrefu kupita,” alisema Stela Mwenigoha mmoja wa washiriki wa sherehe za maadhimisho ya siku ya Wanawake, kupitia Kongamano hili la Wanawake wa Kanda ya Kati
Pia Kamati za ulinzi wa mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto, wazee, wanawake na wenye ulemavu kuanzia ngazi ya taifa hadi vijiji zimeonyesha kufanya kazi kwa kusuasua kutokana na ufinyu wa bajeti, huku nyingi zikiwa zimekufa na hakuna tija yoyote katika utendaji wake hali inayozidisha idadi ya matukio ya ukatili kwa watu kufanya chochote bila hofu, hasa maeneo ya vijijini
“Mtoto anabakwa hadi anakuja kujulikana unakuta tayari ana mimba ya miezi sita, kiukweli inasikitisha wazazi hawapo kabisa karibu na watoto wao, na hata hizo kamati kuna nyingine zinafanya kazi zinaibua matukio lakini hakuna kinachoendelea,” anasema Mwedinuu Kassim
|