Mjumbe wa bodi ya Wakurugenzi wa Kondoa Community Network (KCN), Antony Diallo akiongea wakati akifungua mafunzo yaliyoandaliwa na taasisi ya Kondoa Community Network (KCN) ya kuelimisha matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwa vikundi mbalimbali vya kujiletea maendeleo yaliyofanyika hivi karibuni Wilayani Kondoa, Dodoma.
Mwenyekiti wa taasisi ya Haki Maendeleo, Wilfred Warioba akitoa mada kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii katika mafunzo yaliyoandaliwa na taasisi ya Kondoa Community Network (KCN) yaliyofanyika hivi karibuni Wilayani Kondoa, Dodoma.
Mjumbe wa bodi ya Wakurugenzi wa Kondoa Community Network (KCN), Antony Diallo (kulia) akijadiliana jambo na Mwenyekiti wa taasisi ya Haki Maendeleo, Wilfred Warioba (kushoto). Katikati ni Rebecca Mwimbi, Mmoja wa watoa mada katika mafunzo hayo.
………………………………………………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu
Wananchi wameshauriwa kufanya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, Whatsapp, Instagram, Youtube na Tweeter na kujiepusha na vitendo vya usambazaji wa habari za uzushi na upotoshaji huku akionya kufanya hivyo ni uvunjifu wa sheria zinazosimamia matumizi ya mitandao hiyo nchini.
Rai hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa taasisi ya Haki Maendeleo, Wilfred Warioba katika mafunzo yaliyoandaliwa na taasisi ya Kondoa Community Network (KCN) ya kuelimisha matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwa vikundi mbalimbali vya kujiletea maendeleo yaliyofanyika hivi karibuni Wilayani Kondoa, Dodoma.
Akiongea katika mafunzo hayo, Warioba alisema kuwa pamoja na fursa nyingi zinazopatikana katika mitandao ya kijamii lakini bado kumekuwa na changamoto ambazo zinazojitokeza wakati wa kubadilishana taarifa katika mitandao hiyo.
Warioba ambaye alikuwa mmoja wa wawezeshaji wa mkutano huo alisema kuwa ni muhimu wananchi kuchukua tahadhari pindi wanapokuwa wanabadilishana taarifa zao mitandaoni kwa kufanya hivyo itawasaidia kupunguza athari zinazotakana na watu wenye nia mbaya.
Aliongeza kuwa kupitia mitandao hiyo ya kijamii watu wenye nia ovu wamekuwa wakitumia vibaya mitandao hiyo kwa kusambaza habari za uzushi na upotoshaji jambo ambalo limekuwa likizusha taharuki kwa jamii.
Aliendelea kusema kuwa kufanya vitendo hivyo ni kosa na pindi mtu anayesambaza habari za uzushi na upotoshaji akikamatwa atashitakiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Ni vyema mtumiaji wa mitandao ya kijamii anapopata taarifa yoyote kutafuta uthibitisho kuhusu ukweli wa taarifa hiyo kabla ya kuisambaza ili kupunguza taharuki kwa jamii na kujiepusha na uvunjifu wa sheria inayosimamia mitandao hiyo nchini”, alisema Warioba
Aidha, Warioba alisema kuwa mitandao hiyo ya kijamii imeleta fursa nyingi za watu kujitafutia maendeleo yao kwani kupitia mitandao hiyo kuna jukwaa kubwa la kupata taarifa mbalimbali zinazoweza kukusaidia kupiga hatua kimaendeleo.
Wakiongea katika mafunzo hayo, washiriki waliziomba mamlaka husika na usimamizi wa mitandao hiyo kuweka mifumo mizuri ya kulinda taarifa za watumiaji kwani hivi karibuni kumeibuka watu wenye nia ovu ambao wanapigia simu watu na kutoa taarifa za uongo kwa lengo la kutaka kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu.
Katika miaka ya hivi karibuni mitandao ya kijamii imekuwa ni kitovu cha upatikanaji wa habari nchini na duniani kote ambapo kuibuka kwa mitandao hiyo kumeleta mapinduzi makubwa katika tasnia ya habari, changamotoiliyopo ni baadhi ya watu kutumia vibaya mitandao hiyo.