Baadhi ya Wanafunzi wa Shule za Sekondari wakipita mbele ya mgeni rasmi (hayupo pichani) wakiwa na mabango yenye jumbe mbalimbali katika sherehe za uzinduzi wa Mkakati wa Miaka mitano (2020 – 2025) wa kukabiliana na mimba za utotoni mkoa wa Rukwa.
Wanafunzi wa Shule za Msingi wakipita mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (aliyepo jukwaani) katika sherehe za uzinduzi wa Mkakati wa Miaka mitano (2020 – 2025) wa kukabiliana na mimba za utotoni mkoa wa Rukwa.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akisalimiana na wananfunzi wa shule ya Sekondari Kizwite kabla ya kuwazawadia fedha baada ya kutumbuiza kwa wito unaohamasisha ilinzi kwa watoto katika sherehe za uzinduzi wa Mkakati wa Miaka mitano (2020 – 2025) wa kukabiliana na mimba za utotoni mkoa wa Rukwa.
Wanafunzi wa shule ya Msingi majengo wakitoa burudani mbele ya mgeni rasmi mkuu wa mkoa wa Rukwa (hayupo pichani) kwa wimbo wao wa kuhamasisha kumjali na kumpatia haki mtoto katika sherehe za uzinduzi wa Mkakati wa Miaka mitano (2020 – 2025) wa kukabiliana na mimba za utotoni mkoa wa Rukwa.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (mwenye suti nyeusi) akitiliana saini mkataba wa Mkakati wa kukabiliana na mimba za utotoni Mkoa wa Rukwa kuanzia mwaka 2020 hadi 2025 na Wakuu wa Wilaya tatu za mkoa huo mbele ya wabunge wa mkoa (nyuma ya Mkuu wa Mkoa).
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akimkabidhi Mkakati wa kukabiliana na mimba za utotoni Mkoa wa Rukwa kwa mwaka 2020 hadi 2025, Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Julieth Binyura kwaajili ya kutekeleza na kusimamia yaliyomo katika mkakti huo wakati wa Uzindizi wa mkakati huo pamoja na kuuanza mwaka wa mtoto kwa mkoa.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akimkabidhi Mkakati wa kukabiliana na mimba za utotoni Mkoa wa Rukwa kwa mwaka 2020 hadi 2025 Mbunge wa Viti maalum CHADEMA Mh. Aida Khenan kwaajili ya kusimamia na kutekeleza yaliyomo katika mkakati huo wakati wa shereze za uzinduzi wa mkakati huo.
…………………………………………………………………………………………………….
Katika kuhakikisha mwaka wa 2020 unakuwa maalum kwaajili ya kuwajali na kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyopelekea mimba za utotoni, lishe duni, ulawiti, kukosa elimu, na pamoja na aina mbalilmbali za manyanyaso anayoyapata mtoto, mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaasa wananchi wa mkoa huo kuhakikisha wanawachuja wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya mkoa huo kupitia sera zao juu ya kutetea maslahi ya watoto pamoja na haki zao katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
Amesema kuwa msingi bora wa makuzi ya mtoto ni elimu na mkoa wa Rukwa wenye vijiji 339 na Kata 97, kuna vijiji 59 havina shule za msingi na kata 25 hazina shule ya Sekondari hali inayowapelekea wananfunzi kutembea umbali zaidi ya kilometa 5 kwenda shule hali inayosababisha kurubuniwa kwa wepesi na hatimae kupata mimba za utotoni na kuongeza kuwa pamoja na vijiji na kata hizo kukosa shule viongozi wa maeneo hayo wapo ikiwemo maafisa watendaji wa vijiji na kata, madiwani na wabunge pamoja na viongozi wa vyama vyote vya siasa.
“Mwaka jana tumefanya uchaguzi wa serikali za mitaa, sasa jukumu lao la kwanza hawa viongozi na hao wengine ambao wanataka kuwa wabunge mwaka huu, na madiwani wahakikishe kwamba hivi vijiji 59 vyote vinakuwa na shule ya msingi, kampeni zenu kujipanga kwenu kote, piga ua jengeni shule za msingi kwenye vijiji vyenu vyote 59, na kule ambako kuna shule ya msingi hakikisheni kuna vyumba vya madarasa vya kutosha pamoja na madawati, hapo ndio tutakuwa tunawatendea haki wananchi, lakini sio tunatafuta uongozi wakati huduma za jamii zimedumaa, hili ni jukumu kubwa kwa yeyote yule anayetangaza nia au kwa anayetaka kubaki kwenye nafasi yake ya ubunge na udiwani” Alisisitiza.
“Watoto wanakaa kwenye nyumba ambazo sio rasmi kama mabweni au hosteli wanajipangisha huko, halafu wanajilea, mtoto mdogo ametoka darasa la saba ambaye miaka yote amekuwa akilelewa na wazazi wake lakini ghafla anaanza kujilea mwenyewe, ajilishe ajipikie, aoge, ajilinde mwenyewe tunawapeleka wapi hawa, kwahiyo ni lazima tujenge mabweni, tujenge shule za sekondari kwenye kata zote 25 hili ni jukumu jingine la viongozi hawa wapya wa serikali za mitaa wakishirikiana na wakurugenzi, madiwani na wabunge wanaotangaza nia, hili ni jukumu kubwa na muwahoji huko, akifika huko unamwambia hatuna shule ya sekondari katika kata yetu, tutashirikiana namna gani tujenge shule ya sekondari kwenye hii kata?” Alisema
Aidha, Mh. Wangabo amewaagiza wakuu wa wilaya kuhakikisha shule zote zinatoa chakula shuleni bila ya kujali kama ni uji wa subuhi ama chakula cha mchana na wafanye hivyo na kushirikiana na wakurugenzi, wazazi, kamati za shule na kusisitiza kuwa viongozi hao watapimwa kila baada ya miezi mitatu na kila mwaka ili watoto wapate chakula shuleni na kuzingatia elimu.
Mh. Wangabo ameyasema hayo katika sherehe za uzinduzi wa mkakati wa miaka mitano (2020 – 2025) wa kukabiliana na mimba za utotoni katika mkoa wa Rukwa jana tarehe 18.2.2020 tukio lililofanyika katika mji mdogo wa Namanyere, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi na kuhudhuriwa na wabunge wa mkoa huo, Wakurugenzi, Wenyeviti wa halmashauri pamoja na wadau wa maendeleo kwa mtoto ikiwemo Plan International.
Wakati akisoma risala mbele ya mgeni rasmi kwa niaba ya watoto wenzie mwanafunzi Alsiegarce Bernad alimuomba Mkuu wa Mkoa huyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kusimamia utekelezaji wa mkakati huo ili watoto wa mkoa wa Rukwa waweze kupata haki zao stahiki na kuongeza kuwa kupitia mwaka 2020 kuwa ni mwaka wa mtoto, hivyo watoto wanatarajia kwamba wazazi ama walezi kutekeleza wajibu wa kuwapatia mahitaji yao ya msingi ikiwemo kuwaandikisha shule na kufuatilia maendeleo yao shuleni.
“Kuhakikisha mtoto anaweza kujifunza na kusaidia kazi za nyumbani zisizo athiri elimu, afya na zinazoendana na uwezo wa mtoto, kuwalinda watoto dhidi ya unyanyasaji, unyonywaji, kutelekezwa, kufanyiwa ukatili na kuchukua hatua pale ambapo haki za mtoto zimevunjwa, kushirikiana na serikali na wadau wengine katika kuhakikisha huduma zinapatikana kwa viwango stahiki katika maeneo yao.” Alisema.
Halikadhalika katika uzinduzi huo ulitoka ushuhuda wa aliyekuwa mwanafunzi Shule ya Sekondari Mtenga, Wilayani Nkasi ambaye alipata ujauzito akiwa kidato cha nne na kukimbiwa na aliyempa ujauzito bila ya mafanikio ya kumpata na hatimae alijifungua na hivi sasa anaendelea na ulezi huku akitegemewa na mdogo wake anaemsomesha.
“Baada ya hapo mradi wa Plan ulifika pale Kijiji cha mtenga, nilijiunga na kuchagua fani ya ushonaji, nilijifunza ushojani na nikajua na tuliwezeshwa vifaa vya ushonaji, hadi sasa najua kushona najipatia fedha zinazokidhi mahitaji yangu, hata hivyo nina mdogo wangu anasoma, na sasa hivi ananitegemea mimi kuniomba fedha za matumizi shuleni, Namshukuru Mkuu wa mkoa kutoa elimu juu ya utokomezaji wa mimba za utotoni, asanteni,” Alisema.
Kwa upande wake mbunge wa viti maalum wa CHADEMA mkoani Rukwa Mh. Aida Khenan aliwataka wanafunzi wanaopata ujauzito wakiwa shuleni kutokata tamaa kwani hata yeye ni muhanga watukio hilo wakati alipokuwa kidato cha tatu na leo hii ni mbunge na hivyo kuwataka wananchi wa mkoa wa Rukwa kuungana pamoja kutokomoeza mimba za utotoni.
“Mkutano sio wangu, Wilaya ni ya kwetu, mabadiliko ni ya kwetu, wito wangu kwa wazazi, malezi ya mtoto yanaanza kwetu sisi wazazi, yanafuata kwa mwalimu na jamii inayotuzunguka, Wilaya ya Nkasi tumekuwa kinara sasa kwa mimba za utotoni katika mkoa wa Rukwa, sio sifa nzuri sana na sisi wenyewe wana Nkasi tuna uwezo wa kufanya mabadiliko tukiongozwa na mimi mwenyewe na wanankasi wengine, Kwasababu Rukwa ni pamoja na Wilaya ya Nkasi,” Alisisitiza
Awali akielezea mikakati ya shirika la Plan International kaimu meneja wa shirika hilo mkoa wa Rukwa Kisasu Sikalwanda amesema kuwa shirika limejipanga kuboresha elimu kwa jamii kupitia mijadala mbalimbali itakayofanyika katika ngazi za kata kwa viongozi wa dini, viongozi wa kata, wazee mashuhuri pamoja na watu maarufu kwa lengo la kuzungumza habari ya unyayasaji na ukatili wa kijinsia unaoendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini na hasa katika mkoa wa Rukwa
“Leo hii tunakubaliana na wewe pamoja na mkakati huu unaokwenda kuuzindua kwa jitihada mabzo tunatarajia kuzifanya na hasa mwezi huu wa tatu, tunataraji kutoa elimu kwa kamati zisizopungua 33 katika kata mbalimbali katika mkoa wa Rukwa na hatimae malengo yetu ni kuja kuwafikia viongozi mbalimbali takriban 660 kutoka kata 33 katika mkoa wetu wa Rukwa, Pia kama Plan International mwezi wa tatu tunataraji kupata mradi utakaolenga kupambana na mimba za utotoni na uzazi wa mapema” Alisema.
Awali akitoa maelezo mafupi juu ya mkakati huo Mganga mkuu wa mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu alisema kuwa mimba za utotoni na uzazi katika umri mdogo ni miongoni mwa changamoto zinazoukabili Mkoa.
“Takwimu za utafiti wa kidemografia za mwaka 2015-2016 zinaonyesha kuwa asilimia 29 ya wanawake wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi19 katika Mkoa tayari ni wajawazito au wameshazaa. Kiwango hiki ni kikubwa ikilinganishwa na kiwango cha kitaifa ambacho ni asilimia 27. Tafsiri ya hali hii ni kuwa, katika Mkoa wa Rukwa, Wanawake 29 kati ya wanawake 100 wenye umri wa miaka 15 hadi 19 ni wajawazito au tayari wamezaa,” Alisema.
Na kuongeza kuwa sababu zinazopelekea mimba za utotoni ni pamoja na kutokuwajibika kwa wazazi na viongozi katika suala zima la ulinzi na usalama wa mtoto hasa mtoto wa kike, uelewa mdogo wa jamii kuhusu sheria zinazosimamia masuala ya mahusiano ya watoto na wanafunzi, ukatili wa kijinsia, shinikizo rika, idadi ndogo ya shule za bweni na idadi ndogo ya shule zinazotoa huduma ya chakula cha mchana kwa wanafunzi.
Takwimu za matukio ya mimba za utotoni katika Mkoa zinaonyesha kuwa, kwa kipindi cha miaka mitatu (2017 hadi kufikia Agosti, 2019), jumla ya matukio 722 ya wanafunzi kupata mimba yaliripotiwa ambapo kati ya hao, matukio 171(24%) yalitokea katika Shule za Msingi na matukio 551(76%) yalitokea katika Shule za Sekondari huku kwa mwaka 2019 peke kukiwa na mashauri 692 ya ukatili dhidi ya watoto. Mwaka huu wa Mtoto unaongozwa na Kauli mbiu isemayo “Ulinzi na Usalama wa Mtoto ni Jukumu la Kila Mmoja Wetu.”