Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akizungumza na
Watendaji Wakuu wa Jeshi la Polisi Nchini, katika ukumbi wa mikutano wa Jeshi
hilo, jijini Dar es Salaam, leo. Simbachawene amewataka viongozi hao
wawakikishe wanawahoji watuhumiwa waliopo katika mahabusu ya vituo vya
polisi nchini ili kujua makosa waliyoyafanya kama wanastahili kuwepo katika
mahabusu hizo. Kushoto ni Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (wapili kushoto),
akimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Bajeti, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa
Polisi, Justus Kamugisha, alipokuwa anazungumza katika Kikao cha Watendaji
Wakuu wa Jeshi la Polisi Nchini, kilichofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Jeshi
hilo, jijini Dar es Salaam, leo. Simbachawene amewataka viongozi hao
wawakikishe wanawahoji watuhumiwa waliopo mahabusu ya vituo vya polisi
nchini ili kujua makosa waliyoyafanya kama wanastahili kuwepo katika
mahabusu hizo, akiwa na lengo la kudhibiti wanaobambikiziwa kesi. Kushoto ni
Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kulia), akimsikiliza
Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro alipokuwa anazungumza katika Kikao
cha Watendaji Wakuu wa Jeshi la Polisi Nchini, kilichofanyika Ukumbi wa
Mikutano wa Jeshi hilo, jijini Dar es Salaam, leo. Simbachawene amewataka
viongozi hao wawakikishe wanawahoji watuhumiwa waliopo katika mahabusu ya
vituo vya polisi nchini, ili kujua makosa waliyoyafanya kama wanastahili kuwepo
katika mahabusu hizo, akiwa na lengo la kudhibiti wanaoambikiziwa kesi.
Kushoto ni Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kushoto)
akizungumza na Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro, kabla ya kuanza kikao
cha Watendaji Wakuu wa Jeshi la Polisi Nchini, kilichofanyika katika ukumbi wa
mikutano wa Jeshi hilo, jijini Dar es Salaam, leo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kushoto) akimuaga
Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro, baada ya kumaliza kikao cha Watendaji
Wakuu wa Jeshi la Polisi Nchini, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa
Jeshi hilo, jijini Dar es Salaam, leo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (katikati meza kuu),
akizungumza na Watendaji Wakuu wa Jeshi la Polisi Nchini, katika ukumbi wa
mikutano wa Jeshi hilo, jijini Dar es Salaam, leo. Simbachawene amewataka
viongozi hao wawakikishe wanawahoji watuhumiwa waliopo katika mahabusu ya
vituo vya polisi nchini na kufanya mchujo kwa kuwahoji watuhumiwa waliopo
katika vituo mbalimbali vya polisi nchini, ili kujua makosa waliyoyafanya kama
wanastahili kuwepo katika mahabusu hizo. Kushoto ni Inspekta Jenerali wa
Polisi, Simon Sirro. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
……………………………………………………………………………………………………..
Na Felix Mwagara, MOHA
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amewataka Watendaji
Wakuu wa Jeshi la Polisi wawahoji watuhumiwa waliopo katika mahabusu ya vituo vya
polisi nchini ili kujua makosa waliyoyafanya kama wanastahili kuwepo katika mahabusu
hizo.
Waziri Simbachawene amesema lengo lake kuu la agizo hilo ni kudhibiti ubambikizwaji
kesi ambao upo katika vituo mbalimbali nchini ambapo baadhi ya watuhumiwa
wanapelekwa magerezani kwa makosa ambayo hawakuyafanya.
Akizungumza katika kikao chake na Watendaji hao kilichofanyika ukumbi wa ofisi
ndogo ya Makao Makuu ya Jeshi hilo, jijini Dar es Salaam, leo, Waziri Simbachawene
alisema maelekezo yake pamoja na ya Rais John Magufuli yanahusu masuala ya kesi
na ubambikizaji wa kesi ambayo yapo katika baadhi ya vituo vya Polisi nchini.
“Nawataka mfanye mchujo katika kesi za watuhumiwa mbalimbali waliopo mahabusu
ambazo zinapelekwa mahakamani watuhumiwa hao wanafanyiwa ‘screening’ hata
mara mbili au tatu kwa kuwahoji makosa yao uso kwa uso ili kuhakikisha mtuhumiwa
huyo ndiye mwenye kesi ya mauaji, au anakesi ya kubaka, au anakesi ya wizi, na hata
akipelekwa mahakamani awe ndiye anayestahili,” alisema Simbachawene.
Simbachawene ameongeza kuwa, kunaweza kutokea wakati mwingine mtuhumiwa
anakuwa na kesi nyingine lakini anapewa kesi ambayo hastahili na m tuhumiwa huyo
anashangaa kwa kuwa sio kosa alilolitenda ambalo kakamatwa nalo.
Pia Waziri Simbachawene, aliwataka Viongozi hao wa Polisi kusimamia kwa hekima na
busara suala la vijana wengi wanaoendesha bodaboda, kwa kuwa ni kundi kubwa na
vijana ambao wamejiajiri kwa lengo la kupambana na ukosefu wa ajira nchini na
duniani kwa ujumla.
“Isitafsiriwe kwamba ukiwaona vijana waenda bodaboda ni watu wa hovyo hovyo,
waendesha bodaboda wapo wenye digrii, diploma, kidato cha sita, wenye vyeti, wapo
kidato cha nne, sio kundi la hovyo kama wanavyofikiri baadhi ya watu, hawa ni watu
waliojiajiri na wanafanya shughuli zao kihalalikwa mujibu wa sera za nchi, kwa hivyo ni
lazima tutambue mchango wao na pia tutambue changamoto zao,” alisema
Simbachawene.
Alisema Jeshi la Polisi linapaswa kuwa makini, na litumie busara na uadilifu na pia liwe
na huruma katika kuwaangalia vijana hao waendesha bodaboda ambao wanahangaika
kutafuta riziki na kuendesha maisha yao.
Aliongeza kuwa, Taifa na dunia kwa ujumla kuna ukosefu mkubwa wa ajira hivyo
kunapotokea vijana wanajiari lazima eneo hilo litunzwe na lipendwe na sio
kupachukulia eneo la kukomeshana kwa kuwanyanyasa na kuwafanya kama
hawatakiwi katika jamii.
Aidha, Waziri Simbachawene aliwataka watendaji hao waendeleze ushirikiano walionao
ili kuweza kupata njia ya mafanikio zaidi katika utendaji wa Jeshi hilo.
“Hii nyimbo yenu ya maadili kwa kweli nimeependa, na ninatamani kila mwananchi
ajifunze, ni mzuri na unalengo jema, hivyo wimbo huu nawataka muuishi kutokana na
wimbo unavyotaka, lazima tuwe na maadili mema na tuliendeleze Jeshi letu la Polisi,”
alisema Simbachawene.
Kwa upande wake, Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro, alimshukuru Waziri huyo
kwa kufanya kikao na viongozi wa Jeshi lake, na alimuahidi kwa kushirikiana na
viongozi wenzake, watayafanyia kazi maagizo yote aliyoyatoa.
“Tumefurahi kumpokea Mheshimiwa Waziri hapa Makao Makuu Madogo ya Polisi, ni
mara ya kwanza kufika hapa, na pia amezungumzia mambo mengi, yakiwemo maadili
ya kazi, na pia amezungumza masuala ya uhalifu, amesema tupambane na uhalifu
mapema kwa kuzuia kabla ya kutokea, na pia amezungumza masuala ya kushirikiana
ndani ya Jeshi, na pia amezungumzia masuala ya bodaboda, na tunaahidi maagizo
yote aliyoagiza tutayafanyia kazi,” alisema Sirro.
Waziri Simbachawene tangu ateuliwa na Rais Magufuli kuiongoza Wizara hiyo, baada
ya aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, kangi Lugola, kuondolewa katika nafasi hiyo,
ameanza ziara ya kutembelea taasisi za wizara yake ambazo ni Jeshi la Polisi, tayari
amezungumza nao, na anatarajia kufanya kikao na Jeshi la Magereza, Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa.