Baadhi ya Wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakimsikiliza
Naibu Waziri wa Madini, Mhe.Stanslaus Nyongo wakati wa Mkutano wake na
wahariri wa vyombo vya habari nchini leo katika Ofisi ndogo za Wizara hiyo Jijini
Dar es Salaam, kuhusu mkutano mkubwa Wa Madini utakaofanyika katika Kituo cha Mikutano Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Tanzania kuanzia Februari 21 hadi 23,2020.
Naibu Waziri wa Madini, Mhe.Stanslaus Nyongo, akizungumza na wahariri wa Vyombo vya Habari Nchini (pichani), leo katika Ofisi ndogo za Wizara hiyo Jijini Dar es Salaam, kuhusu mkutano mkubwa Wa Madini utakaofanyika katika Kituo cha Mikutano Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Tanzania kuanzia Februari 21 hadi 23,2020.
Naibu Waziri wa Madini, Mhe.Stanslaus Nyongo, akizungumza na wahariri wa Vyombo vya Habari Nchini (hawapo pichani), leo katika Ofisi ndogo za Wizara hiyo Jijini Dar es Salaam, kuhusu mkutano mkubwa Wa Madini
utakaofanyika katika Kituo cha Mikutano Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Tanzania kuanzia Februari 21 hadi 23,2020.
Picha na Idara ya Habari-MAELEZO
*********************
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya kufunga mkutano mkubwa wa sekta ya madini utakaoambatana na utoaji wa cheti cha umahiri kwa madini ya bati utakaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam Jumamosi wiki hii.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam leo, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amesema mkutano huo wa aina yake utafungua fursa kwa wadau wa madini wakiwemo wafanyabiashara ,watafiti na hata wawekezaji wakubwa kuja kuchangamkia fursa
zilizosheheni katika sekta hiyo hapa nchini.
“Mkutano huo wa wadau ni muhimu sana kwani utaambatana na maonyesho ya shughuli mbalimbali za
sekta ya madini na utatoa fursa kwa wadau kuongeza wigo wa kupanua biashara ya madini, na pia
utafanyika uzinduzi rasmi wa cheti cha umahiri kwenye madini ya bati” Alisema Naibu Waziri.
Alisema cheti cha umahiri ni nyenzo muhimu katika sekta ya madini, kwani nchi yetu itatambulika rasmi
duniani kama wazalishaji wa madini hayo hivyo kuwa na utambulisho mahsusi hasa madini hayo
yanapokuwa yameuzwa katika nchi za nje.
Naibu Waziri Nyongo amesema kupatikana kwa cheti hicho ni kutokana na Tanzania kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini pamoja na jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kuhakikisha rasilimali madini zinalinufaisha taifa na wananchi wake kwa ujumla.
Amesema Tanzania iliridhia itifaki ya kimataifa ya udhibiti wa uuzaji wa madini ambapo madini yanatakiwa yajulikane yalikochimbwa, yalivyosafirishwa na hata thamani yake ili kudhibiti vitendo vya kuibuka kwa vikundi vyenye silaha, vinavyopambana na serikali hasa katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kwingineko ambapo madini imekuwa chanzo kikubwa cha fedha za kununulia silaha na kufadhili vikundi hivyo.
Mkutano huo wa siku mbili utaambatana pia na kuwasilishwa kwa mada mbalimbali zinazohusu sekta ya
madini zitakazowasilishwa na wadau na wasomi mahiri katika sekta ya madini akiwemo Profesa Shukrani
Manya, Profesa Hamis Mruma pamoja na Profesa mahiri kutoka nchini Kenya katika chuo Kikuu cha
Nairobi P.L.O Lumumba.
Tangu Serikali ya Awamu ya Tano Kuingia Madarakani mwaka 2015 sekta ya madini imeanza kuzaa
matunda kwa kuliingizia taifa fedha nyingi kutokana na udhibiti wa utoroshaji wa madini, ujenzi wa
ukuta katika machimbo ya Tanzanite Mirerani mkoani Manyara , pamoja na ujenzi wa masoko ya madini
katika kila mkoa na baadhi ya Wilaya.