****************************
Na Ahmed Mahmoud,Arusha
Kaya masikini zinazoishi katika kata ya Olbalbal wilayani Ngorongoro zimepatiwa mbuzi na kondoo 624 watakaowasaidia kupunguza kiwango cha umasikini na kujipatia mahitaji muhimu pamoja na kujiendeleza kiuchumi.
Wananchi hao kutoka kaya zenye kipato duni wakizungumza katika makabidhiano ya mbuzi hao waliotolewa na kikundi cha Narikungishu kilichopo boma la utamaduni la ,Indemwa lililopo katika kata hiyo ,John Ngeka na Nalepo Emanuel walisema kuwa mifugo hiyo itawawezesha kupata kipato cha uhakika ,licha ya kutegemea shughuli za ufugaji na utalii wa utamaduni bado wataongeza kipato chao kupitia ufugaji.
John Ngeka alisema kuwa atatumia mbuzi hao na kondoo katika kuongeza tija ya ufugaji na kujipatia kipato kutokana na mifugo kwa ili aweze kubadilisha maisha yake na familia yake.
Diwani wa kata hiyo Emmanuel Tonge alisema kuwa kwa kipindi cha mwaka jana walitoa mbuzi 300 lakini kwa mwaka huu wametoa mbuzi 624 ili kuinua kipato cha maisha ya kaya masikini ziweze kujimudu na kukua kiuchumi.
“Mbuzi hawa na kondoo tunawagawa kwa kaya masikini ili ziweze kujikwamua kiuchumi badala ya kuwapa fedha tunawapa mifugo ili waweze kuifuga izaliane na kuongezeka na kuwaongezea kipato kitakachowainua kiuchumi” alisema Emmanuel
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Rashid Taka alisema kuwa licha ya uwezeshaji huo wanapaswa kulinda utamaduni wao ambao umekua chanzo cha utalii kupitia utalii wa utamaduni na kuonya baadhi ya watu wanaoiba utamaduni na ubunifu na kuufanya bila kufuata sheria na taratibu .
Taka aliyataka maboma ya utamaduni kuiga mfano wa boma hilo kwa kuwawezesha wananchi wanaozunguka kata hiyo ili waweze kunufaika na matunda ya utalii wa utamaduni.