Home Mchanganyiko WANANCHI WAFURAHIA UJENZI WA ZAHANATI

WANANCHI WAFURAHIA UJENZI WA ZAHANATI

0
………………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Wananchi wameonyesha kufurahishwa na kitendo cha Serikali kuendeleza ujenzi wa Zahanati ambazo zilisimama ujenzi kwa muda mrefu.
Hayo yamejitokeza kwenye ziara aliyoifanya Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu ya kufuatilia ujenzi wa Zahanati ya Mitondi iliyopo Kijiji cha Mitondi B kata ya Kitama pamoja na Zahanati ya Miuta iliyopo Kijiji cha Miuta kata ya Miuta ambapo alikuta ujenzi ukiendelea kwa kasi hali inayowafurahisha Wananchi kiasi cha kuamua kujitoa kusimamia miradi hiyo bure kwani walikuwa na kiu kuona ukamilifu wake ili waanze kupata huduma kwa ukaribu zaidi.
Zahanati ya Mitondi B imeanza kujengwa mwaka 2008 hadi mwaka 2017 uliposimama ujenzi ambao umegharimu Tsh. Milioni 28 nguvu za Wananchi na ujenzi wake sasa upo usawa wa upauaji bati; Na mradi wa ujenzi Zahanati ya Miuta ulianza kwa nguvu ya Wananchi Tsh. Milioni 5 na baadae Serikali kuwaunga mkono Wananchi kuuendeleza na leo ujenzi unaendelea kwa kuwekwa marumaru na kupigwa rangi hali inayowafurahisha Wananchi wengi.
*”Miradi hiyo  imeanzishwa kwa nguvu za Wananchi na Serikali ilikuja baadae kuwaunga mkono. Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Magufuli ipo kazini kuhakikisha inaendeleza mapambano dhidi ya adui maradhi. Nimeona furaha ya Wananchi wakishuhudia na kusimamia miradi hiyo mara baada ya Serikali kuwapa fedha za kuiendeleza. Rai yangu kwa Wananchi wasimamie miradi hiyo vyema kwa kuhakikisha ubora wa ujenzi unaendana na thamani ya fedha. Wakandarasi pia nimewasisitizia waongeze kasi ya ujenzi ili ikamilike kwa ubora, mapema na kwa wakati.”* Alisisitiza Gavana Shilatu wakati akizungumza mara baada ya ziara hiyo ya ufuatiliaji ujenzi wa miradi hiyo ya Zahanati.
Kwenye ziara hiyo Gavana Shilatu aliambatana na uongozi wa kata, uongozi wa Serikali ya Kijiji pamoja na kamati za miradi hiyo.