TANZANIA imepangwa katika Kundi D pamoja na Zambia, Guinea na Namibia kwenye Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), zinazotarajiwa kuanza Aprili 4 hadi 25 mwaka huu, zikihusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.
Chini ya kocha Mrundi, Etienne Ndayiragije Taifa Stars imefuzu CHAN ya mwaka huu, ikiwa ni mara ya pili tu kihistoria kwao baada ya kuzitoa Kenya na Sudan kufuatia kucheza fainali hizo kwa mara ya kwanza mwaka 2009 nchini Ivory Coast.
Katika droo iliyopangwa leo ukumbi wa Palais Polyvalent des Sports de Yaounde, Jijini Yaounde, wenyeji, Cameroon wamepangwa Kundi A pamoja na Zimbabwe, Mali na Burkina Faso.
Washindi mara nyingi zaidi wa taji hilo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambao wamebeba Kombe hilo mara mbili, wao wamepangwa Kundi B dhiri ya jirani zao, Kongo Brazaville, mabingwa wa 2014, Libya na Niger.
Mabingwa watetezi, Morocco wao wamepangwa Kundi C pamoja na Togo watakaoshiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza, Rwanda na Uganda.
Simba Wasiofungika watashiriki fainali za CHAN kwa mara ya nne wakijaribu kuvunja rekodi zao za msimu iliyotangulia, ambazo ni kufika Robo Fainali mara mbili nchini Sudan mwaka 2011 na Rwanda 2016.
Timu nyingine katika Kundi A, Burkina Faso, inacheza kwa mara ya tatu fainali hizo na Mali walifungwa kwenye fainali na DRC mwaka 2016.
Morocco watarajie upinzani kutoka kwa wawakilishi wa Afrika Mashariki, Uganda ambao walikosa fainali za kwanza tu pamoja na mwanachama mwingine wa CECAFA, Rwanda.
Togo wao wamefuzu kwa mara ya kwanza kabisa kwenye fainali za CHAN, wakiwatoa Nigeria walioingia fainali mwaka 2018 katika hatua ya mwisho wa mchujo.