Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.William Lukuvi,akitia saini hati miliki kwaajili ya Manispaa ya Kigamboni baada ya kukabidhi ekari 715 Manispaa hiyo.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.William Lukuvi, akimkabidhi hatimiliki ya ardhi Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni Bw.Ng’wilabuzu Ludigija.
********************************
NA EMMANUEL MBATILO
Serikali kupitia wizara ya ardhi imekabidhi hati ya umiliki wa eneo la ekari 715 halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni ili kuweza kutumika katika shughuli za kuwahudumia wananchi wa manispaa hiyo.
Akizungumza na wanahabari katika makabidhiano hayo Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.William Lukuvi, amesema kuwa upangaji wa matumizi ya eneo hilo lazima uzingatie masharti na sheria za nchi na kwamba litumike kujenga ofisi zote za kuhudumia jamii ikiwemo Hospitali, Mahakama, Nyumba za watumishi wa halmashauri hiyo ili iwe rahisi kwa wananchi kuzifikia huduma.
Aidha amesema tayari serikali imeshaanza uchunguzi wa ofisa ardhi aliyedaiwa kuomba fedha wananchi ili awahudumie na pia amewataka watumishi wanaojihamisha kiholela kukimbia madudu yao, warudishwe katika ofisi walizopangiwa kwa utaratibu wa kiserikali wakajibu tuhuma zinazowakabili.
“Sisi tunajua kuwa kuna mtumishi anaomba pesa wananchi yaani anajilipa mwenyewe, tena tuna ushahidi hivyo ameanza kuchunguzwa ili tukithibitisha tumchukulie hatua za kisheria,” amesema Mhe.Lukuvi.
Hata hivyo Mhe.Lukuvi amesema katika upangaji wa matumizi ya eneo hilo Wilaya ihakikishe inazingatia maslahi ya umma na lisigawiwe kwa mtu mmoja mmoja, hiyo itasaidia wananchi kwani hapo ni katikati mwa wilaya hiyo.
“Tunajua mamlaka ya upangaji wa matumizi ya eneo ipo chini ya wilaya husika hivyo lazima muhakikishe mnazingatia maslahi ya umma kwani eneo hili lipo katikati ya wilaya hivyo ni vyema wananchi wakapata huduma zote hapa,”Amesema Mhe.Lukuvi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni Bw.Ng’wilabuzu Ludigija, amesema pamoja na kupokea hati hiyo, pia watahakikisha wanafuata matakwa ya sheria katika upangaji wa matumizi.
Pamoja na hayo amesema kuwa katika manispaa hiyo kumekuwa na changamoto kadhaa za ardhi ambapo maeneo mengi yamepimwa lakini hayajamilikishwa hivyo serikali haipati kodi yake huku maeneo mengine yakiwa hifadhi ya wahalifu kutokana na kuwa mapori makubwa.
Aliiomba serikali iwasaidie kukabiliana na changamoto hizo ili Manispaa hiyo iwe na hali shwari.
Ikumbukwe kuwa hatua ya Waziri Lukuvi, ya kukabidhi eneo hilo kwa manispaa ya Kigamboni ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk. John Magufuli, aliyemtaka kufanya hivyo baada ya eneo hilo kurudi katika umiliki wa serikali.
Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, eneo hilo limerudi kwa serikali baada ya Rais Dk. John Magufuli, April 9, mwaka 2017 kufuta hati ya mmiliki wa awali ambaye ni kampuni ya International Village Limited ambayo ni kampuni tanzu ya Quality Group, kutokana na kushindwa kulihudumia kwa takribani miaka 10.
Dk. Magufuli alitoa siku saba eneo hilo liwe limekabidhiwa kwa Manispaa ya Kigamboni, kuanzia Februari 10, mwaka huu, alipokuwa katika hafla ya kuzindua majengo ya manispaa hiyo.