***********************
Happy Lazaro,Arusha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ACP Jonathan Shana amemkanya Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema kuacha tabia ya kupenda kutafuta mtaji wa kisiasa katika masuala yanayohusu uchumi na uzalendo wa nchi.
Kamanda Shana ameyasema hayo leo katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari.
Kauli hiyo imetokana na maagizo aliyoyatoa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya Usalama Mkoa huo kwa jeshi la Polisi mkoa wa Arusha, kuwatafuta wale wote waliosambaza picha zenye kuonyesha uharibifu wa miundombinu ya barabara katika eneo la Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro.
“Nimeona Mhe Lema Mbunge wa Arusha Mjini anasema atashangaa kuona watu wakikamatwa kwa Uchochezi, natumia fursa kumtahadharisha akae mbali na suala hili wakati huu ambao Jeshi kabambe lipo kazini kuhakikisha Mkoa unaendelea kuwa Salama na Utalii unashamiri” ilisema taarifa hiyo.
Aidha Kamanda Shana alibainisha umuhimu wa Sekta ya Utalii nchini na kusisitiza kwamba yeyote atakayeonekana kuikwamisha sekta hii atashughulikiwa kama Mhujumu Uchumi.
Kamanda Shanna kupitia taarifa hiyo,alisema kuwa,jeshi la polisi limepokea maelekezo ya Mhe Mrisho Gambo ambaye ni mkuu wa mkoa wa Arusha na Mwenyekiti kabambe ya usalama mkoa ,ya kuhakikisha wachochezi wote pamoja na wanaochafua taswira nzuri ya nchi yetu wanakamatwa Mara moja nasi tumelipokea agizo hili na tutatekeleza kwa asilimia Mia moja .
Alifafanua kuwa,jeshi Hilo litahakikisha linawasaka kila Kona ya mkoa na mahali popote walipo bila kujali nafasi zao walizonazo.
“Namshauri mbunge Lema asikariri na asome alama za nyakati maana hii si awamu ya mchezomchezo naamini kwa pamoja tunaweza ,uzalendo wetu Kwanza na siasa baadaye.”alisema Kamanda Shanna.
“Utalii unachangia 17.5% ya pato lote la Taifa, Utalii unachangia 25% ya fedha zote za kigeni, Ngorongoro mapato yake ni 143 Billion kwa mwaka, Ngorongoro inatoa gawio la Serikali kiasi cha 23.5 Billion kwa mwaka, Mapato ya Tanapa ni kiasi cha Bilioni 282.42 kwa mwaka,hili ni suala linalohusu uchumi wa nchi yetu kwa hiyo wanasiasa wasilete siasa wala masihara kwenye uchumi wa Nchi” ilisema taarifa hiyo.
Kamanda Shana amesisitiza Jeshi la Polisi Mkoani Arusha linaendelea kufanya upelelezi wa wale wote waliohusika na uhalifu huo na mara watakapobainika watafikishwa katika vyombo vya dola.