…………………………………………………………………………………………………………….
AJALI YA MAGARI MAWILI KUGONGANA NA KUSABABISHA MAJERUHI NA UHARIBIFU.
Mnamo tarehe 17.02.2020 majira ya saa 03:00 usiku wa kuamkia leo huko eneo la Ilomba, Kata ya Ilomba, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya katika barabara kuu ya Mbeya – Tunduma, Gari lori tanker la mafuta lenye namba za usajili T.720 DHV na Tela T.520 CCY likiendeshwa na ABUBAKAR MOHAMED [36] Mkazi wa Dar es Salaam likitokea Dar es Salaam kuelekea nchini Zambia likiwa limebeba mafuta Petrol na Diesel liligongana uso kwa uso na Gari ndogo yenye namba za usajili T.536 DEM aina ya Toyota Carina iliyokuwa ikiendeshwa na EMMANUEL CORNEL @ FUNGO [45] Mfanyabiashara na Mkazi wa Uyole iliyokuwa inatokea Mbeya Mjini.
Katika ajali hiyo dereva wa gari ndogo T.536 DEM Toyota Carina amepata majeraha sehemu za shingoni, mgongoni na kiunoni na anaendelea na kupatiwa matibabu Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya. Chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa magari yote mawili katika eneo la makazi ya watu. Aidha katika ajali hiyo magari yote mawili yameharibika na Tanker la Mafuta liliacha njia na kwenda kugonga maduka/vibanda vya bidhaa mbalimbali vilivyopo kando kando ya barabara.
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vipo eneo la tukio kuhakikisha mafuta yaliyopo katika gari lililopata ajali yanahamishiwa kwenye gari lingine bila kusababisha madhara yoyote ikiwa ni pamoja na jitihada za kuliinua tanker la mafuta lililoacha njia na kupinduka.