************************
NA EMMANUEL MBATILO
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Innocent Bashungwa anatarajia kuwa mgeni rasmi katika mashindano ya nne ya KAIZEN kitaifa yatakayofanyika tarehe Februari 18 mwaka huu kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Lengo la mashindano hayo ni kuwezesha wadau kubadilishana uzoefu sambamba na kumpata mshindi atakayewakilisha Tanzania kwnye mashindano ya KAIZEN barani Afrika yatakayofanyika Afrika Kusini Septemba mwaka huu.
Mashindano hayo yatafuatiwa na sherehe za kukabidhi tuzo kwa washindi zitakazoanza saa 8 mchana. Hata hivyo mashindano yanatarajiwa kuhudhuriwa na jumla ya washiriki 150 wakiwemo wazalishaji wa viwandani, washauri waelekezi, viongozi na maafisa wa serikali na wakufunzi wa KAIZEN, Wanahabari, wawakilishi kutoka Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Taasisi ya sekta binafsi (TPSF), Jumuiya ya Wenye Viwanda na Kilima Tanzania (TCCIA), Jumuiya ya Wanawake Wafanyabiashara Nchini (TWCC).
KAIZEN ni falsafa kutumia mbinu bunifu ya uimarishaji endelevu wa tija na ubora viwandani ambayo inazingatia usimamizi na matumizi bora ya rasilimariwatu, fedha, muda na miundombinu ili kupunguza upotevu wa gharama zisizokuwa za lazima viwandani na hatimaye viwanda vyetu kuweza kuhimili ushindani wa biashara.