****************************
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Februari 10, 2020 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya uamuzi ufuatao;
Ligi Kuu ya Vodacom:
Mechi namba 178: Simba SC 2 v Coastal Union
FC 0
Kocha wa Simba Steven Vanden Broeck amepewa Onyo Kali kwa kosa la kugoma kuwafungulia mlango mwamuzi na Kamishina wa mchezo wakati wa ukaguzi wa timu katika mechi hiyo iliyochezwa Februari 01,2020 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni namba 41(13) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Makocha.
Mechi namba 188: Simba SC 2 VS Polisi Tanzania FC 1
Klabu ya Polisi Tanzania imepigwa Faini ya kiasi cha Tsh.1,500,000/=(Milioni Moja na Laki Tano) kwa kosa la kutumia mlango usio rasmi wa kuingia Uwanjani katika mechi iliyochezwa Februari 04,2020 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo
Vile vile katika mchezo huo Kocha Mkuu wa Klabu ya Simba Sc Steven VandenBroeck ametozwa Faini ya kiasi cha Tsh.500,000/=(Laki Tano) kwa kosa la kugoma kuongea na waandishi wa habari mara baada ya mchezo kumalizika.Adhabu hii ni kwa kuzingatia Kanuni namba 41(12) kuhusu Udhibiti wa Makocha.
Mechi namba 189:Azam Fc 1 vs Tanzania Prisons Fc 1
Mchezaji wa Klabu ya Azam Fc Agrrey Moris amepigwa Faini ya kiasi cha Tsh.200,000/=(Laki Mbili) kwa kosa la kugoma kuongea na waandishi wa habari mara baada ya mchezo kumalizika katika mechi iliyochezwa Februari 05,2020 katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.Adhabu hii imetolewa kwa mujibu wa Kanuni namba 38(18) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.
Mechi namba 190:Yanga Sc 2 vs Lipuli Fc 1
Mwamuzi Abubakar Mturo amefungiwa miezi mitatu(3) kwa kosa la kushindwa kumudu mchezo katika mechi iliyochezwa Februari 05,2020 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni namba 39(1) ya Ligi Kuu Kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.
Vile vile katika mchezo huo mwamuzi msaidizi namba mbili Joseph Pombe amefungiwa miezi mitatu(3) kwa kosa la kushindwa kumudu mchezo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni namba 39(1) ya Ligi Kuu Kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.
Mechi namba 191:Simba SC (0) vs JKT Tanzania (1)
Mwamuzi msaidizi namba mbili Kassim Mpanga Amefungiwa miezi mitatu(3) kwa kosa la kushindwa kutafsiri sheria za mpira wa miguu katika mechi iliyochezwa Februari 07,2020 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni namba 39(1) ya Ligi Kuu Kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.
Pia katika kikao hicho Kamati iliielekeza Sekretarieti kufuatilia viongozi wa vilabu na Makocha ambao hivi karibuni wamekuwa wakishutumu na kutoa matamshi yenye kukashifu na kudhalilisha viongozi ,Chapa (Brand) ya Ligi na Taasisi kwa ujumla kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwa vipindi tofauti tofauti.Viongozi na Makocha waliobainika ni wafuatao Kocha wa Klabu ya Namungo FC(Hitimana )-kwenye mchezo wa Simba SC na Namungo Fc, Kocha wa Klabu ya Young African Sc (Luc Aymael)-kwenye mchezo wa Yanga Sc na Lipuli, Msemaji wa Klabu ya Simba SC (Haji Manara) na Muhamasishaji wa Young African sc(Anthonio Nugaz) .
Kutokana na matamshi hayo wanapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF).