**************************
Na Ahmed Mahmoud,Arusha
Serikali ya Tanzania imemuonya vikali mtu anayejiita Nabii Namba saba ambaye jina lake halisi ni Mosses Mollel kuwa itamchukulia hatua kali iwapo atashindwa kuthibitisha madai kuwa na uwezo wa kutibu virusi Vya ugonjwa wa Corona .
Nabii huyo ambaye taarifa zake zilianza kusambaa mwishoni mwa wiki iliyopita kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii akidai anayodawa ya kutibu ugonjwa hatari wa Corona ulioanzia nchini China na kusababisha Vifo Vya watu zaidi ya 1100 hadi sasa,ametakiwa kujisalimisha wizara ya afya na kuthibitisha taarifa hizo.
Akiongea na Vyombo Vya Habari jijini Arusha,Naibu Waziri wa Afya,Dkt Faustine Ndugulile ameeleza kuwa anazo taarifa za Nabii huyo kujitangaza kuwa anayodawa ya kutibu ugonjwa huo na kumtaka athibitishe kauli yake
“Kimsingi nimeiona hiyo taarifa ya huyo mtu anayejiita Nabii Saba kuwa anayo dawa ya kutibu ugonjwa wa Corona ,ila hapa kwetu Tanzania hatuna maambukizi yoyote ya ugonjwa huyo ,tunachotaka huyo mtu atuthibitishie uwezo wake wa kutibu huyo ugonjwa wa Corona” Amesema Ndugulile
Ameongeza kuwa iwapo atashindwa kuthibitisha atachukuliwa hatua Kali za kisheria.
Amesema hadi sasa Serikali imetuma wataalamu wake kwenda kumsaka na kumhoji kama anavyo vibali Vya kutoa huduma ya Tiba na kujitangaza kuwa anatoa Huduma ya kutibu ugonjwa huo hatari ambao hadi sasa mataifa bado yanahaha kusaka Tiba ya ugonjwa huo.
Nabii Namba Saba ambaye ni mkazi wa Ngaramtoni Wilayani Arumeru,Mkoani Arusha amekuwa akijitangaza kuwa anayo dawa ya kutibu ugonjwa huo wa corona na kuweka mawasiliano yake kwenye mitandao .
“Ninayodawa hapa Arusha ya kutibu virusi Vya Corona inayowaua Wachina na mataifa mengine. ” sauti ya Nabii huyo.