……………………………………………………………………………………………..
POLISI TAZARA
Wananchi wanaoishi katika maeneo yote inapopita reli ya Tazara wametakiwa kutunza na kuheshimu miondombinu ya hiyo na kuwafichua watu wanaoihujumu miundombinu ili iendelee kusaidia kuinua uchumi wa Taifa.
Hayo yalisemwa na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Tazara, Kamishna Msaidizi wa Polisi( ACP) Advera Bulimba wakati wa ziara ya kimafunzo katika mitambo ya kuzalisha kokoto na mataruma ya reli kilichopo eneo la Kongoro jijini Mbeya.
Kamanda Bulimba alisema kuwa kumekuwepo na tabia kwa baadhi ya wananchi kujihusisha na vitendo vya uhalifu vya kung’oa na kuiba miundombinu ya reli kna kwenda kuuza kama vyuma chakavu jambo ambalo linadhoofisha utendaji wa reli ya Tazara.
“Madhara ya kuhujumu reli ni makubwa na yanaweza kugharimu maisha ya watu na kusababisha ulemavu wa kudumu, jambo hilo halitakubalika chini ya uongozi wa kikosi cha Polisi Tazara” alisema Kamanda Bulimba
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa reli ya Tazara Fuad Abdala akiwa ziarani humo aliwataka wafanyakazi wa kiwanda cha kuzalisha kokoto na mataruma ya reli kutumia vizuri na kuitunza mitambo hiyo iliyonunuliwa ili iweze kutumika kwa muda mrefu.
Aliwataka wafanyakazi wa kiwanda hicho kuendelea kufanya kazi kwa kujituma na kutunza mitambo hiyo kwa kuwa kiwanda hicho ndiyo roho ya Tazara katika kuimarisha miundombinu ya reli.
Meneja Mkuu wa Tazara, Fuad Abdala alisema, lengo la ziara hiyo ilikuwa kuangalia utekelezaji wa maazimio ya ziara ya mwezi Februari, mwaka jana na kuongeza kuwa ameridhishwa na utendaji kazi wa kiwanda hicho na kuahidi kuendelea kutatua changamoto za wafanyakazi na kiwanda kwa ujumla.