Home Biashara TBS YATOA SEMINA KWA TAASISI ZA KISERIKALI 

TBS YATOA SEMINA KWA TAASISI ZA KISERIKALI 

0

************************

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetoa semina kwa taasisi za Serikali zinazojihusisha moja kwa moja na uondoshaji wa shehene na mizigo bandarini kwa lengo la kulinda afya, usalama, mazingira, ulinzi na ustawi kwa Watanzania.

 

Mafunzo hayo yamekuja baada ya kikao kilichofanyika Novemba 11 hadi 20 mwaka jana baada ya kuonekana baadhi ya taasisi za Serikali zilizopewa jukumu la kuondoa shehena na mizigo bandarini zinachelewesha kazi hiyo
na kusababishia usumbufu na gharama kubwa kwa wateja.

 

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa ufunguzi wa semina kwa taasisi hizo za serikali, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt.Yusuf Ngenya alisema semina hiyo inalenga kutoa elimu juu ya mifumo ya udhibiti wa bidhaa zinazoingia nchini, usajili wa bidhaa zinazoingia nchini na namna ya kufanya maombi kwa njia ya mtandao.

 

Dkt. Ngenya alisema miongoni mwa taasisi zilizoshiriki semina hiyo ni pamoja na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikali ni (GPSA).

 

“Lengo ni kuwapa fursa na kutilia mkazo suala la uondoshaji wa shehena na mizigo bandarini,”alisema.

 

Alisema Shirika hilo lina majukumu manne ikiwemo kuweka na kusimamia viwango vyote vya kitaifa, kutoa mafunzo na ushauri viwandani juu ya uzalishaji wa bidhaa bora, kupima na kuhakiki vipimo vinavyotumika viwandani na kuelimisha umma juu ya masuala yote yanayohusu uwekaji na usimamiaji wa viwango na uthibiti wa ubora wa bidhaa.

 

Kwa upande wake Afisa Udhibiti Ubora wa TBS, Athuman Kisumo, alisema miongoni mwa mada zilizotolewa katika semina hiyo ni pamoja na usajili wa bidhaa zinazoingia nchini,namna ya kufanya maombi kwa njia ya mtandao na majadiliano juu ya changamoto za uondoshaji wa shehena za mizigo bandarini.