Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi Sospeter Magesse (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kaliua – Abel Busalama mashuka. Katikati ni Mkurugenzi wa Wilaya hiyo Dkt. John Pima akishuhudia.
Mkuu wa Wilaya ya Kaliua – Abel Busalama (mwenye suti ya udhurungi)) na baadhi ya viongozi wa Wilaya wakikagua vifaa vilivyotolewa na Benki ya NMB kwa ajili ya hospitali ya Kaliua.
…………………………………………………………………………………………………….
KATIKA kuhakikisha inasaidia na kutatua baadhi ya changamoto zinazoikumba Sekta ya Afya na Elimu Mkoani Shinyanga, Benki ya NMB imetoa msaada wa vifaa tiba, madawati, mbao, mabati, vitanda na Magodoro vyenye jumla ya Sh. milioni 35.
Vifaa hivyo vilipokelewa na kukabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga – Zainab Telack kwa zahanati ya Old Shinyanga iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga. Zahanati hiyo iliyopokea; vitanda vitano vya wagonjwa, magodoro matano na mashuka 62 pamoja na Zahanati ya Usule iliyopo halmashauri ya Shinyanga iliyopokea vitanda vinne, magodoro manne na mashuka 57, huku wakikabidhi pia madawati 100 kwa shule ya msingi Mwenge.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga – Zainab Telack alisema kuwa mahitaji ya miundombinu katika sekta ya Elimu na Afya ni makubwa, hivyo akaishukuru benki ya NMB kwa msaada huo.
Kwa upande wake Meneja wa benki ya NMB Kanda ya Magharibi – Sospeter Magesse alisema kila mwaka wanatenga zaidi ya Sh. Bilioni 1 kusaidia jamii, ambapo ameahidi kuendelea kushirikiana na serikali kama mdau wa maendeleo kuzishika mkono zahanati, shule na vituo vya afya kwa mahitaji mbalimbali.
Magesa pia alieleza kwamba kwa mwaka 2019 NMB imetoa jumla ya Sh milioni 110 kwa Mkoa wa Shinyanga katika kusaidia mahitaji mbalimbali katika sekta ya elimu na afya, huku akiahidi kusogeza huduma za benki hiyo karibu na wananchi ambapo wanatarajia kufungua tawi katika eneo la Iselamagazi zilizohamia ofisi za halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Dk. Amosi Mwenda alisema kuwa msaada huo utasaidia kupunguza mahitaji makubwa waliyonayo hususan kwa akina mama wajawazito, ambapo wako kwenye ujenzi wa hospitali ya halmashauri inayohitaji vifaa mbalimbali.
#NMBKaribuYako