Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akipata maelezo kutoka kwa kwa Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Tabora Eng. Raphael Mlimaji (aliyevaa sweta), wakati alipokagua athari za mvua katika miundombinu ya barabara ya Ipole – Rungwa (km 172) ambayo imekatika katika maeneo manne na hivyo kusababisha mawasiliano ya mikoa hiyo kutokuwepo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Sikonge waliokwama kusafiri kutokana na mvua kubwa kunyesha na kukata mawasiliano ya barabara inayounganisha mkoa wa Tabora na Mbeya.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Ipole – Rungwa (km 172) iliyokatika kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha wilayani Sikonge, mkoani Tabora.
Mwakilishi wa Kampuni ya Western Construction anayekarabati barabara ya Ipole – Rungwa (km 172) Eng. Saidi Nassoro, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, ya kukagua hali ilivyo ya miundombinu ya barabara iliyoathiriwa na mvua, mkoani Tabora.
……………………………………………………………………………………………………………..
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, amemtaka mkandarasi wa kampuni ya Western Construction anayekarabati barabara ya Ipole – Rungwa yenye urefu wa kilometa 172 kwa kiwango cha changarawe kujaza kifusi cha mawe katika maeneo yote yaliyokatika katika barabara hiyo.
Barabara hiyo inayounganisha mkoa wa Tabora na Mbeya ina umuhimu sana katika masuala ya usafiri na usafirishaji wa mazao na bidhaa na tokea mvua zianze kunyesha maeneo manne katika barabara hiyo yamekitika.
Naibu Waziri Kwandikwa ametoa kauli hiyo alipokutana na wananchi waliokwama katika barabara hiyo kwa muda siku mbili wakati akikagua hali ya miundombinu ya barabara mkoani Tabora ambao una jumla ya kilometa 2,153 za barabara kuu na mikoa ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza kuwa Serikali ipo kwa ajili ya kuhudumia wananchi kwa kuwapatia miundombinu mizuri ili kuwezesha uchumi kupanda.
“Mkandarasi fanya kazi usiku na mchana ili mawasiliano yarudi katika maeneo haya ili wananchi waweze kupita huku tukisubiri maji yakipungua na utaratibu wa kujenga maboksi kalvati makubwa uanze”, amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.
Aidha, ametoa wito kwa wasimamizi wa barabara ambao ni Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kusimamia kikamilifu ujenzi wa makalvati yanayoenda sambamba na mahitaji ya maeneo husika kwa siku za usoni ili kutoruhusu tena maji kupita juu ya barabara.
Ameongeza kuwa mpango wa Serikali ni kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili kuwaunganisha wananchi wa mikoa hiyo na kuinua uchumi wa maeneo hayo na maeneo jirani.
“Niwatoe hofu wananchi kwani itakuwa ni historia kwa maeneo yote ambayo yamechelewa kupata mtandao wa barabara za lami hasa kwa upande huu wa mikoa hii ya Tabora, Katavi na Kigoma kwani wakandarasi wapo katika hatua mbalimbali za ujenzi”, amefafanua Naibu Waziri huyo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Kampuni ya Western Construction anayekarabati barabara hiyo, Eng. Saidi Nassoro, ameahidi ndani ya siku hizo mbili kukamilisha zoezi la uwekaji mawe katika maeneo yote yaliyokatika na magari kuruhusiwa kupita tena.
Ameendelea kueleza kuwa barabara hii ilikuwa katika hali nzuri na hii dharura iliyojitokeza haikuwepo na haikutarijiwa kutokana na mvua zile za kawaida hivyo baada ya mvua kunyesha kwa wingi usiotarajiwa na maji mengi kujaa hadi barabarani kukasababisha kukatatika kwa baadhi ya maeneo.
Naye Bi. Semeni Juma, mkazi wa Kitunda wilayani Sikonge ameiomba Serikali kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafiri, muda na gharama za maisha kushuka kulinganisha na sasa.
Naibu Waziri Kwandikwa yupo katika ziara ya kikazi mkoani Tabora ya kukagua athari za mvua zinazoendelea kunyesha hapa nchini na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara.