………………………………………………………………………………………………
NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO
MAKAMU Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mbarouk Salum Mbarouk, amewaasa maofisa waandikishaji wilayani Bagamoyo,mkoani Pwani kuhakikisha wanalipa uzito unaostahili zoezi la kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura na kulifanya kwa umakini mkubwa ili liweze kufanikiwa kwa asilimia 100.
Ametoa rai hiyo wakati, alipofika katika mafunzo maalum kwa maofisa waandikishaji wa wananchi katika uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, yaliyofanyika kwa siku mbili ,na kuhusisha jumla ya waandikishaji wasaidizi 137 na wasimamizi wa mashine za uandikishaji “BVR” .
Jaji Mbarouk alisema Zoezi hili la uboreshaji wa daftari la kudumu ni zoezi la kitaifa na lilizinduliwa rasmi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa huko Mkoani Kilimanjaro mnamo Mwezi Julai, 2019.
Akifungua mafunzo hayo ofisa mwandikishaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Fatuma Latu, alieleza, zoezi la uandikishaji Wananchi kwa Halmashauri ya Wilayani Bagamoyo litaanza februari 14 na kukamilika februari, 20 katika vituo mbalimbali vilivyopo kwenye kata na Vitongoji Wilayani humo.
Aidha, Latu aliwasihi washiriki hao kuhakikisha wanatunza siri, pia kutunza vifaa vyote vitakavyotumika katika zoezi hilo kwani vimenunuliwa kwa gharama kubwa, na kuzingatia maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ili yawasaidie katika utekelezaji wa zoezi hilo .
Akaongeza,”kuwa ana hakika baadhi yao walibahatika kushiriki katika zoezi la uboreshaji wa daftari la orodha ya wapiga kura lililofanyika mwishoni mwa mwaka jana kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za mitaa hivyo wana uzoefu katika uratibu na kusimamia utekelezaji wa uandikishaji wa wapiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Latu alieleza kwamba,serikali ya Wilaya hiyo imedhamiria kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi na ameomba ushirikiano mkubwa kati ya watendaji wote ,serikali, vyama vya siasa, na wadau .
Uboreshaji wa wapiga kura utahusisha Wapiga kura wapya wenye umri wa miaka 18 na zaidi ambao 2015 hawakuandikishwa au wale ambao wamefikisha miaka 18,ambao wamepoteza kitambulisho cha kupiga kura cha zamani au kitambulisho kimeharibika na wanaohamisha taarifa zao kutoka Wilaya au mikoa mingine.