Katibu tawala wa mkoa wa kigoma Rashid Mchata akimkabidhi Mkurugenzi Msaidizi idara ya afya-TAMISEMI baadhi ya miongozo aliyokabidhiwa kutoka wizara ya afya kwa ajili ya utekelezaji
…………………………………………………………………………………………….
Na. Catherine Sungura-Kigoma
Katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko isiingie nchini,wizara ya afya,maendeleo ya jamii, jinsia,wazee na watoto imekabidhi vifaa viwili vya kupima joto la mwili (thermal scanner).
Akikabidhi vifaa hivyo Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa serikali inaimarisha ufuatiliaji wa wasafiri hasa wanaoingia nchini kutoka nchi mbalimbali, lengo ikiwa kuendelea kuzuia magonjwa ya mlipuko yasiingie nchini.
“Licha ya kufanya ukaguzi wa hali ya utoaji huduma za afya pia tumeona tuongeze nguvu kwa mkoa huu ili muweze kuimarisha ukaguzi kwenye kiwanja cha ndege na mipaka yenu”.Alisema Dkt. Chaula
Aidha, Dkt. Chaula alisema kuwa nchi mbalimbali duniani zimekumbwa na magonjwa ya mlipuko, kuna Ebola na hivi sasa Corona imeripotiwa kusambaa katika maeneo mengine” hivyo sisi tunaangalia jinsi gani mkoa wa Kigoma wamejiandaa kujikinga, kuzuia magonjwa hayo yasiingie nchini hivyo vifaa hivi vitaongeza nguvu “.
Alisema kuwa vifaa hivyo vina uwezo wa kutambua joto la mwili na kama linakuwa juu linatoa ishara wataalamu wa afya na hivyo kuweza kuchukua tahadhari ya kumuhudumia muhisiwa.
Hata hivyo alisema tayari Wizara hiyo ilishatoa mafunzo kwa watumishi katika mkoa huo pamoja na kuipatia vifaa maalum vya ukaguzi na kujikinga na kwamba hatua ya kuwapatia vifaa vingine ni kuzidi kuwapa uwezo wa kujiimarisha katika kuyazuia magonjwa hayo
“Pamoja na kukabidhi vifaa hivi, pia tutatembelea na kukagua vituo vya afya ambavyo vipo kwenye ukarabati hivi sasa na maduka ya dawa (ya Serikali), tutakwenda kuangalia namna dawa zetu zinavyodhibitiwa na kutunzwa,” alisema.
Sambamba na hilo, Dk. Chaula alimkabidhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Rashid Mchatta miongozo mbalimbali kwa ajili ya utoaji wa huduma za afya ikiwamo ule wa matibabu kwa wagonjwa wa figo na wenye matatizo ya usikivu.
Naye Katibu Tawala wa mkoa huo alimshukuru Dk. Chaula kwa kumkabidhi vifaa na miongozo hiyo kwani itasaidia kuimarisha mkoa huo katika kuzuia magonjwa hayo yasiingie nchini pamoja na kuboresha huduma za afya kwa wananchi.