Wazazi na walezi wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2020 na hawajaripoti katika shule walizopangiwa wamepewa wiki moja kuhakikisha wanafunzi hao wanaripoti na kuanza masomo kabla ya kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezaria Makota wakati wa kikao cha wadau wa Elimu kwa ajili ya kujadili mafanikio na changamoto za elimu katika Halmashauri kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kondoa Irangi hivi karibuni.
“Wazazi iko shida kwenu mwanafunzi haendi shule na haumuulizi anapaswa kupigwa fimbo au mwanafunzi mtoro anakuja kumchongea mwalimu kwa mzazi badala yake mzazi anakuja juu kwa mwalimu hii si sawa tuache kulea watoto kama mayai tutawaharibu,”alisema Mhe. Sezaria
Aidha aliwataka Maafisa Elimu Kata kufanyakazi zao kwa weredi kwani baadhi yao wameonekana wazembe kwa kutotimiza majukumu yao hivyo ili kufuta dhana hiyo ni jukumu lao kujituma katika nafasi zao na kuwasihi kuacha kuwapakazia ubaya Maafisa Elimu kwani wanafanya kazi zao vizuri na matokeo yanaonekana.
“Niwapongeze pia wakuu wa Shule ya Sekondari ya Kwapakacha na Shule ya Wasichana Kondoa kwa kujituma na kufanya kazi vizuri kwani matokeo yanaonekana ikiwa ni pamoja na Walimu Wakuu wa Mpalangwi, Kondoa Islamic na viongozi wa Wilaya na tukiendelea kushirikiana nina imani tutafikia malengo ya kupandisha elimu ya watoto wa Kondoa,”alisisitiza Mhe. Makota.
Akiongea katika kikao hicho Mwenyekiti wa Halmshauri ya Mji Wa Kondoa Mhe. Hamza Mafita alisema kuwa ili kuondokana na matatizo ya elimu katika Halmashauri ni kuanzisha Mfuko wa Elimu ambao utasaidia kupunguza changamoto zinazoikabili Elimu ambapo kila kata itapewa fedha kulingana na jinsi walivyochangia ili kutatua changamoto zinazowakabili.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kondoa aliwashukuru wadau kwa kujitokeza kwa wingi na kutoa mawazo chanya kwa lengo la kuboresha elimu ya mtoto wa Kondoa kwani maendeleo ya Kondoa yataletwa na wote walioshiriki kikao na wenye dhamana ya kuwahudumia wana Kondoa.
“Pamoja na yote kuanzia sasa ni marufuku Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule kuitwa Wilayani mara kwa mara kwani kunawafanya washindwe kusimamia majukumu yao iwapo Idara ina maagizo wafuateni hukohuko mashuleni ikiwa ni pamoja na walimu wote na viongozi kufuata Sheria, Taratibu na Kanuni za utumishi wa Umma na kushirikiana na viongozi, wazazi na wanafunzi wote ili kuinua elimu,”aliongeza Mkurugenzi Dakawa.
Mmoja wa wadau kutoka Mtaa wa Hachwi ikiwa ni moja ya Shule zilizofanya vibaya Bw. Salim Bura alisema kuwa kwasasa wanajamii ya Hachwi wameamka na kuona umuhimu wa Elimu ambapo kwasasa wapo tayari kumpatia nyumba ya kuishi bila malipo Mwalimu atakayepangwa katika Shule Shikizi ya Kotumo na kuiomba Halmashauri kuwafikishia huduma muhimu ikiwemo maji na umeme.
Kikao cha wadau kimeketi ili kujadili mafanikio na changamoto za elimu katika Halmashauri ya Mji wa Kondoa na kilianza kwa kusoma taarifa za Idara za Elimu na maazimio ya vikao vya wadau wa Elimu katika ngazi ya kata na taarifa za Ofisi za Udhibithi Ubora wa Elimu, Chama Cha Walimu na Tume ya Watumishi wa Walimu na kilihudhuriwa na Waheshimiwa Madiwani,wadau wa Elimu, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu, Maafisa Elimu Kata, viongozi wa dini na Wazee maarufu.