Home Mchanganyiko MWENYEKITI WA TUME YA MADINI PROFESA IDRIS KIKULA AANZA ZIARA MOROGORO

MWENYEKITI WA TUME YA MADINI PROFESA IDRIS KIKULA AANZA ZIARA MOROGORO

0

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kushoto) akisalimiana na mmoja wa watendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa MMC mara baada ya kuwasili kwenye eneo hilo lililopo Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro.

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (wa kwanza mbele) akiendelea na ziara yake katika Mgodi wa MMC

Meneja Mgodi wa MMC, Mhandisi Shabani Mpelela (kulia) akielezea namna uchenjuaji wa dhahabu unavyofanyika kwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (katikati)

*******************************

Leo tarehe 11 Februari, 2020 Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula ameanza ziara katika mkoa wa Morogoro ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Njombe na Mbeya (Chunya) yenye lengo la kufuatilia maelekezo aliyoyatoa kwenye ziara yake ya awali, kukagua shughuli za uchimbaji wa madini pamoja na kutatua changamoto mbalimbali za wachimbaji na wafanyabiashara wa madini.

Katika ziara yake mkoani Morogoro, Profesa Kikula aliambatana na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Shija pamoja na wataalam kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro na Makao Makuu ya Tume ya Madini.

Kati ya maelekezo aliyoyatoa Profesa Kikula katika ziara yake ya awali aliyoifanya kuanzia tarehe 29 Oktoba, 2019 hadi tarehe 03 Novemba, 2019 ni pamoja na utoaji wa eimu kwa wachimbaji wa madini ujenzi kuhusu umuhimu wa kuwa na mpango wa utoaji wa huduma kwa jamiii ( corporate social responsibility, CSR), wakaguzi kwenye vituo vya ukaguzi wa madini ujenzi kuwa na vifaa vya kutosha na kufanya kaguzi za mara kwa mara kwenye maeneo yenye shughuli za uchimbaji wa mchanga kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

Malekezo mengine ni pamoja na kuhakikisha wachimbaji wa madini ujenzi wanakuwa na mipango ya ufungaji migodi, wachimbaji wadogo wa madini wasio rasmi kurasimishwa pamoja na kupewa leseni za uchimbaji madini, kuhakikisha wamiliki wa leseni za madini wanaendesha shughuli zako kwa kuwa na mazingira mazuri ya kazi ikiwa ni pamoja na kuzingatia sheria na kanuni za afya na utunzaji wa mazingira na kusimamia bei elekezi za madini zinazotolewa na Tume ya Madini.

Katika hatua nyingine, Profesa Kikula alifanya ziara kwenye Mgodi wa Dhahabu wa MMC uliopo Wilayani Mvomero mkoani Morogoro ambapo mara baada ya kutembelea mgodi huo aliuelekeza uongozi wa mgodi huo kuhakikisha unakamilisha ujenzi wake ili uweze kuzinduliwa mapema na kuanza uzalishaji na Serikali kupata maduhuli yake.

“Serikali kupitia Wizara ya Madini na Tume ya Madini ina kiu ya kuona ujenzi rasmi wa mgodi unakamilika na kuzinduliwa na kuanza kuzalisha hali itakayopelekea ongezeko la mapato katika mkoa wa Morogoro,” alisema Profesa Kikula.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa MMC, Abubakar Mohamed alieleza kuwa, kwa sasa wako katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa ujenzi wa mgodi na kuongeza kuwa watahakikisha mgodi unazinduliwa mapema iwezekanavyo na kuanza kufanya kazi.