Na.Mwandishi Wetu- MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli amezindua Wilaya ya Kigamboni kwa kufungua Jengo la Mkuu wa Wilaya, Jengo la Halmashauri ya Manispaa pamoja na Hospitali ya Wilaya hiyo.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa majengo hayo, Rais Magufuli amesema amefurahishwa na maendeleo makubwa yanayofanyika katika Wilaya hiyo na kwamba Serikali itawabeba wananchi wa Wilaya hiyo ambao kwa muda mrefu wamehangaika kupeleka mazao na bidhaa mbalimbali upande wa pili wa Jiji la Dar es Salaam.
“Maendeleo ya Wilaya hii yatapatikana kwa watu kuchapa kazi nataka ndani ya wiki moja viongozi wote wa wilaya hii wawe wamehamia hapa ili waweze kutoa huduma kwa ukaribu wakiwa hapahapa, na natoa agizo kwa Waziri Mhagama kuwa nyumba za NSSF wapewe viongozi hao tena wakae bure kwa mwaka mmoja” Alisema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli amesema kwakuwa Kigamboni ni kinga ya mboni ya jicho la Dar es Salaam Serikali itahakikisha inapangwa vyema ili ifanane na maeneo mengine yaliyopangwa vizuri kwaajili ya makaazi na uwekezaji kwa manufaa ya maendeleo ya wananchi.
Rais Magufuli amemwagiza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kuhakikisha katika kipindi cha wiki moja umiliki wa ardhi ya eneo la Kigamboni unarudishwa ndani ya miliki ya Manispaa ya Kiganmboni badala ya kuendelea kuwa chini ya Wizara hiyo ili Manispaa ipange matumizi ya maendeleo.
Aidha Rais Magufuli amemwagiza Waziri wa TAMISEMI Selemani Jaffo kutenga shilingi Bilioni 2 kwaajili ya kuanza kujenga nyumba za serikali katika Wilaya ya Kigamboni ili baada ya mwaka mmoja aliowapa watumishi na viongozi wa wilaya hiyo wa kukaa bure katika nyumba za NSSF kumalizika, wawe wanahamia kwenye nyumba za serikali.
Rais Magufuli pia ameeleza kushangazwa kwake na taarifa kwamba Wilaya hiyo imepanga kujenga jengo la kuhifadhia maiti kwa gharama ya shilingi milioni 500 na kuelekeza kama taarifa hiyo ni sahihi mradi huo ufutwe mara moja.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli amemwelekeza Naibu Waziri wa Afya Dkt.Faustine Ndungulile kuhakikisha hospitali ya Wilaya ya Kigamboni inapatiwa Madaktari pamoja na Madawa na vifaa tiba ili ianze kuhudumia wananchi mara moja.
Wakati huohuo Rais Magufuli amewataka watanzania wanaoishi mabondeni kuhama mara moja kwani mvua zinazoendela kunyesha zimeleta maafa kwa watu wengi na kwa mujibu wa mamlaka ya hali ya hewa nchini bado mvua hizo zinaendelea.
“Nawaagiza wananchi wote wa Tanzania waliojenga mabondeni wahame, mabonde yatumike kwaajili ya kulishia mifugo na kilimo tu maana ndugu zangu maji yanakawaida ya kufuata mkondo wake wa asili hivyo mkiendelea kujenga mabondeni mnajitaftia maafa nyinyi wenmyewe na Serikali haitahangaika kusaidia watu wa namna hiyo” Alisema.
Uzinduzi wa Wilaya ya Kigamboni umehusisha Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya lililogharimu Shilingi Bilioni 1.6, Jengo la Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni lililogharimu shilingi Bilioni 5.2 pamoja na hospitali ya Wilaya Shilingi bilioni 1.5. miradi iliyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli.
Katika kipindi cha mwaka 2016 hadi sasa Jumla ya Shilingi Bilioni 33 zimetumika katika kujenga majengo ya wakuu wa Mikoa , wakuu wa Wilaya pamoja na Halmashauri ikiwa ni katika mpango wa serikali wa kuhakikisha huduma zinatolewa katika mazingira rafiki.
Wilaya ya Kigamboni ni Wilaya mpya katika mkoa wa Dar es Salaam iliyozaliwa kutoka katika wilaya ya Temeke ambayo inafanya idadi ya Wilaya katika Mkoa huo kuwa Tano nyingine zikiwa Ubungo, KInondoni pamoja na Ilala.