Tanzania imeunga mkono wazo la kutaka nchi za Kiafrika kuwa na vyanzo mbadala vya fedha ili kukabiliana na majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi na kutoa wito kwa nchi zilizoahidi kuchangia fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi katika mkutano wa Paris kuheshimu ahadi zao.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo katika mkutano wa 33 wa wakuu wa nchi na serikali wa Umoja wa Afrika unaoendelea Addis Ababa, Ethiopia wakati wa mjadala kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na njia za kukabiliana na athari zake na kuzisihi nchi zilizoahidi kutoa michango katika mkutano wa Paris kuhusu mazingira kuheshimu ahadi zao.
Mhe Samia Suluhu Hassani ameongeza kuwa kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa kiasi kikubwa inarudisha nyuma jitihada za maendeleo ya nchi za Afrika kutokana na uharibifu wa miundo mbinu pia vifo vinavyotokana na vimbunga,mafuriko ama ukame unaosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi na kuunga mkono wazo la Nchi za Afrika kuwa na mfuko maalum pamoja na vyanzo mbadala vya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Suala la elimu nalo lilipata fursa ya kujadiliwa katika mkutano huu wa 33 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika ambapo Tanzania imepata nafasi ya kuchangia mjadala huo na kuridhia wito wa kuzitaka nchi zote za Afrika kuongeza bajeti zake katika sekta ya elimu ili kuwawezesha vijana wa kiafrika kupata elimu iliyo bora nay a ushindani.
Taarifa ya mpango wa Nchi za Afrika kujitathmini kiutawala bora yaani APRM,iliyowasilishwa na Mwenyekiti Mpya wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni Rais wa Afrika ya Kusini Mhe. Cyril Ramaphosa ameitaja Zimbabwe kuwa ni mojawapo ya nchi ambazo zimeridhia na kusaini mpango huo jambo ambalo Tanzania kupitia kwa Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Zimbabwe licha ya hali mbaya iliyonayo na mapito inayopitia ikiwa ni pamoja na vikwazo vya kimataifa.
Mkutano huo wa 33 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika umeingia katika siku yake ya pili ukitanguliwa na ule wa Baraza la Mawaziri wa Umoja huo uliofanyika kuanzia Februari 6 hadi 7 mjini Addis Ababa Nchini Ethiopia.