******************************
NA EMMANUEL MBATILO
Serikali imeanza utaratibu wa kuwatambua wafanyakazi wote wanaotoa huduma katika sekta ya Utalii kwa kutoa cheti cha ithibati maalumu cha kuwatambua ili kuhakikisha taaluma ya utalii inazingatiwa na kuongezeka kwa thamani kwenye sekta hiyo.
Ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam Waziri wa maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala katika ufunguzi wa mkutano wa siku mbili wa kimataifa juu ya kuunganisha taaluma ya tasnia ya utalii na ukarimu katika nchi zinazoendelea ambapo amesema kuwa
“Katika Mkutano huu utasaidia kuwepo kwa ongezeko la thamani kwenye sekta ya Utalii hivyo takribani maandiko 52 yatawasiliswa na yatawasaidia wadau wa utalii kubadilishana uzoefu”. Amesema Dkt.Kigwangala.
Ameongeza kuwa serikali imejitahidi kupunguza muda wa upatikanaji wa visa za kuingia nchini kutoka miezi minne mpaka kufiki siku nne hivyo kuwarahisishia watalii kuingia nchini na kuongeza chachu ya kukua kwauchumi wa taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Chuo cha Utalii NCT Dkt. Shogo Mlozi amesema wahitimu wengi hawakidhi mahitaji ya soko na swala hilo ni mtambuka katika sekta mbalimbali nchini na duniani kwa ujumla.
Aidha katika mkutano huo wadau wa sekta ya utalii watapata nafasi ya kukuza ujuzi,kutambua tabia za watalii na mahitaji yao hivyo kusaidia kuwahudumia vema.