Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb)
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo, Rome-Italy
Serikali imewahakikishia wakulima na watanzania kwa ujumla kuwa Tanzania haijavamiwa na Nzige wa Jangwani kama inavyoripotiwa na mitandao mbalimbali ya kijamii.
Kauli ya serikali imetolewa na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Italia Mhe George Kahema Madafa Leo tarehe 10 Februari 2020 mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Flumicino Jijini Rome nchini Italia Mhe Hasunga amesema kuwa kumekuwa na maneno yakienezwa lakini hakuna Nzige wa Jangwani nchini Tanzania.
“Mimi nawahakikishia wakulima na wananchi wenzangu wa Tanzania kuwa kumekuwa na taarifa zinazoenea kwenye baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu uwepo wa nzige wa Jangwani nchini hususani mkoa wa Kilimanjaro siyo za kweli sisi tupo salama” Waziri Hasunga
Ameongeza kuwa hakuna taarifa za kitaalamu zilizothibitisha uwepo wa nzige kwenye mikoa ya Kilimanjaro na Arusha. Ila ni kweli Kuna nzige wameonekana Kaunti ya Kajiado nchini Kenya takribani kilomita 50 toka mpakani na Tanzania” Alisisitiza
Mhe Hasunga ameongeza kuwa Wataalam wa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo duniani (FAO) linaendelea na ufuatiliaji wa viashiria vya uwepo wa nzige na tayari hatua za awali za kuwadhibiti endapo wataingia nchini zimechukuliwa.
Aidha, amesema kuwa hatua hizo ni pamoja na Mashirika ya kimataifa ambayo Tanzania ni wanachama kuiahidi serikali ya Tanzania ndege tatu maalum za kunyunyizia dawa na uwepo wa dawa za tahadhali kwenye mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
Waziri Hasunga ametoa mwito kwa wakulima, maafisa ugani na kilimo na wadau wote wa kilimo kuendelea kutoa ushirikiano wa taarifa sahihi kwa serikali endapo kutajitokeza viashiria vya nzige kwenye maeneo ya mashamba.
MWISHO