NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
WAZIRI wa TAMISEMI ,alhaj Suleiman Jafo, ametoa rai kwa Watanzania waendelee kuidumisha amani kwa kujenga hofu ya mungu ili kuinua maendeleo na uchumi wa nchi.
Aidha ameitaka jamii kujitolea katika masuala ya maendeleo pamoja na kuchangia ujenzi wa nyumba za ibada ili kujiongezea thawabu kwa Allah.
Alhaj Jafo aliyasema hayo ,wakati akikagua ujenzi wa mskiti mpya wa Masjid Quba utakaogharimu sh.milioni 200 kwa awamu ya kwanza ambapo hadi kukamilika itahitajika sh.bil 2.4 huko Mwanalugali, pamoja na kufanyika harambee Kibaha Mjini ,Pwani.
Alieleza ,pale ambapo hakuna hofu ya mungu amani hutoweka hivyo ni vyema watu wakafuata misingi ya dini ili kudumisha amani.
Akimwakilisha Waziri Mkuu, Waziri huyo
alisema sheikh mkuu wa mkoa huo, sheikh Hamis Mtupa amethubutu kwa kuwa uwekezaji huu ni endelevu.
“Kwa kuwa ni uwekezaji wa imani kuna watu wanafanya ibada ,ni uwekezaji endelevu kwa faida na urithi pia wa vizazi vijavyo, :’unaweza kuwa na urithi wa majumba yetu unapata watoto waweza kugeuza jumba madangulo, au wakaja kuuwana kwahiyo urithi huu ni mkubwa”alifafanua alhaj Jafo .
Hata hivyo, Jafo aliendesha harambee ya kuchangia ujenzi huo na kusema ujenzi unaonekana kujengwa kwa viwango na kulingana na thamani .
“Binadamu tunawekeza katika elimu,sherehe ,afya lakini tunasahau kuchangia na kuwekeza katika maeneo ya ibada ambayo ni faida hadi ahera’alisisitiza Jafo.
Akielezea kuhusiana na ujenzi wa mskiti huo, katibu wa ujenzi Saghire Daudi alisema ,jengo litakuwa na ghorofa mbili na awamu ya kwanza wanahitaji sh.milioni 200 na itachukuwa waumini 1,500.
“Kwasasa walikuwa na mskiti mdogo unaochukua waumini 400 hivyo kukamilika kwa mskiti huo utasaidia waumini na kutafuta nguvu kubwa ya nje ,kwani wao wameanza na kuchangishana kiasi cha sh.milioni 110″alieleza Saghire.
Alisema, ujenzi utaendelea baadae na hadi kukamilisha awamu nyingine mbili na wakijaaliwa watamalizia na jumla ya kukamilisha mskiti mzima ni bilioni 2.4.
Saghire aliomba ,wadau na wafadhili wengine wajitokeze kusaidia kuwezesha mskiti huo uweze kumalizika.
Akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Pwani, mkuu wa wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama alieleza taasisi za dini zinashirikiana na serikali kudumisha amani kupitia kamati za dini.
Assumpter alifafanua kwamba, wananchi washirikiane bila kujali imani zao za kidini ili kudumisha amani.
Nae,mwenyekiti wa CCM mkoani Pwani, Ramadhani Maneno alihamasisha wananchi kujitokeza katika zoezi la uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura linalotarajia kuanza februari 14-20 mwaka huu.