**************************
Na Mwandishi Wetu,
Tunduru
UGONJWA wa kifua kikuu unaoenea kwa kasi kubwa hapa nchini, unatajwa kama Bomu linalosubili kuangamiza watu wengi iwapo jamii na wadau mbalimbali hawatashiriki vema katika kampeni ya kutokomeza ugonjwa huo unaotajwa kati ya magonjwa kumi yanayoongoza kupoteza maisha ya Watanzania.
Hayo yamesemwa jana na mratibu wa kifua kikuu na Ukoma kutoka Hospitali ya wilaya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole, katika kampeni na mkakati wa wilaya wa kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu iliyofanyika katika kijiji cha Majimaji wilayani hapa.
Mkasange alisema, hali ya kifua kikuu katika wilaya ya Tunduru bado hairidhishi kwani kuna wagonjwa wengi wenye maradhi hayo wakiwemo watu wanne wenye kifua kikuu sugu kati yao mmoja hajulikani alipokwenda na jitihada za kumtafuta ili aendelee kutumia dawa zinazofanyika.
Alisema,mtu mwenye kifua kikuu sugu matibabu yake ni tofauti na TB ya kawaida kwani mwenye kifua kikuu sugu anatakiwa kutumia dawa kwa miaka miwili mfululizo,tofauti na kifua kikuu cha kawaida ambacho matibabu ni miezi sita.
Alisema, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo shirika la Afya Duniani(WHO) limeweka mkakati wa pamoja kuhakikisha ugonjwa wa kifua kikuu unamalizika ifikapo mwaka 2030.
Mkasange alisema, kwa kutambua ukubwa wa tatizo hilo Serikali itaendelea kutoa matibabu ya ugonjwa huo bure na kuwataka wale wanaobainika kuwa na vimelea vya TB kuhakikisha wanatumia dawa ili kuokoa maisha yao na watu wengine.
Ametaja makundi yaliyopo kwenye hatari ya kupata kifua kikuu ni wasafiri,waliopo kwenye misongamano,wazee watu wenye magonjwa sugu, na wale wenye magonjwa ya muda mrefu kama ukimwi,kansa na wale wanaotumia dawa bila kufuata ushauri wa Daktari.
Katika hatua nyingine Mkasange alisema, kama jamii itafuata kanuni bora za maisha kuna uwezekano mkubwa wa kutokomeza kabisa ugonjwa wa kifua kikuu.
Ameitaka jamii kuwapa ushirikiana waathirika wa ugonjwa huo,kwani mgonjwa wa TB anakuwa hatari sana pale ambapo hajaanza matbabu,lakini aliyeanza dawa sio rahisi kuambukiza wengine.
Kwa upande wake mwakilishi wa shirika la MDH linalofanya kazi na serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya kifua kikuu katika mkoa wa Ruvuma Dkt Nixson John amewahimiza wananchi wa kijiji hicho kujitokeza kwa wingi katika kampeni ya uchunguzi na upimaji wa kifua kikuu ambayo imeanza kuleta tija ya kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo katika jamii.
Amezitaja dalili za mtu mwenye kifua kikuu ni kukohoa kwa muda mrefu,kukohoa damu,kupungua uzito,kutokwa na jasho usiku, na homa za mara kwa mara hivyo kukosa muda wa kushiriki katika kazi za maendeleo.
Dkt John alisema, kampeni ya mwaka huu inafanyika katika utaratibu mpya wa kumfuata mwananchi pale alipo badala ya wataalam kukaa ofisini ambapo alisisitiza kampeni hiyo inalenga kumfikia kila Mtanzania.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika kampeni hiyo walisema,mkakati wa kuwafuata watu majumbani kwa ajili ya uchunguzi wa vimelea vya TB na kupima ni maendeleo makubwa sana katika wilaya ya Tunduru kwani kuna uwezekano mkubwa wa kukomesha kabisa maradhi hayo ikilinganisha na siku za nyuma.
Kangomba Mkuziti amepongeza sana maendeleo yaliyofikiwa kwenye matibabu ya ugonjwa huo kutoka sindano sitini hadi vidonge ambavyo ni rahisi mgonjwa kumeza kwani wapo baadhi ya wagonjwa waliokatisha matibabu ya sindano na wamepoteza maisha.
Kitenge Seleman alisema,kampeni ya nyumba kwa nyumba ni bora sana kwani maeneo ya vijijini kuna watu wengi wenye dalili za ugonjwa huo lakini wameshindwa kufika hospitali kutokana na changamoto za kimaisha ikiwemo kukosa fedha za nauli kumfikisha katika vituo vya matibabu.