*********************************
NA MWAMVUA MWINYI, CHALINZE
DIWANI wa Kata ya Vigwaza ,Mohsin Bharwani ameitaka halmashauri ya Chalinze, kufanyia matengenezo gari ya kubebea wagonjwa ambayo alinunua kwa fedha zake ,zaidi ya sh.milioni 45 lakini haitumiki kwa mwaka mmoja sasa.
Ameeleza gari hiyo, limefanya kazi kwa muda mfupi mara baada ya kuikabidhi halmashauri hiyo miaka miwili sasa.
Akiongea katika kikao cha baraza la madiwani kupitisha bajeti ya mwaka 2020/2021, diwani huyo alisema,ifikie hatua masuala yanayolenga maslahi ya wananchi yasiingizwe na masuala ya kisiasa hali inayosababisha kukwamisha juhudi za wafadhili ama wachache wanaojitolea.
“Kuna wakati nilisikia ina matatizo nikatengeneza, chakushangaza baada ya hapo haifanyi kazi tena ipo tu imepaki “
“Sijapewa taarifa kutoka halmashauri wala jitihada za kutengeneza sizioni, huku kukiwa na kauli kwa baadhi ya watu kuwa gari hii imeharibika baada ya kuwekewa chumvi” alisema diwani huyo.
Diwani Bharwani alieleza,idara ya afya inatakiwa kutenga bajeti kufanya matengenezo ya gari ili ifanye kazi maana ni nzuri haijakongoroka sura ya gari ila tatizo halieleweki hadi leo, ,ila ndio naomba halmashauri isaidie kuchunguza pia kama hiyo chumvi iliwekwa nani ili achukuliwe hatua”
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Saidi Zikatimu alisema suala hilo litafanyiwa kazi ili gari hilo liweze kutengenezwa na watafuatilia taarifa kuhusiana na kuharibika kwake.
Nae mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Mkoani Pwani Ramadhani Maneno,alimuelekeza mkurugenzi kuona namna ya kutengeneza gari hilo lianze huduma kwa wananchi.
Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa, ataketi na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo kujadili suala hilo na watakaobainika kuhujumu gari hilo sisifanye kazi watachukuliwa hatua.