*****************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeboresha utoaji wa huduma za afya kwa kugharamia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vituo 487 vya kutolea huduma za afya.
“Maboresho hayo yanajumuisha vituo vya afya 320, hospitali za halmashauri za wilaya 70, hospitali za zamani tisa na zahanati 88,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Februari 7, 2020) wakati akitoa hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 18 wa Bunge jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Machi 31, mwaka huu.
Mbali na hayo, Waziri Mkuu amesema Serikali imejenga na kuboresha miundombinu ya hospitali za rufaa za Njombe, Simiyu, Mara, Geita, Songwe, Katavi, Sekou Toure, Burigi – Chato, Mwananyamala, na hospitali za rufaa za kanda ya Kusini Mtwara, kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mbeya, hospitali ya Kibong’oto na ujenzi wa Isolation centre katika hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Serikali imekamilisha ujenzi wa nyumba 320 za watumishi wa sekta ya afya pamoja na kugharamia ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kwa gharama ya sh. bilioni 334,” ameongeza.
Amesema katika kipindi hicho, jumla ya madaktari bingwa 311 wameendelea kulipiwa gharama za masomo ya uzamili katika vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi na kwamba, katika kipindi cha nusu ya pili, Serikali inakusudia kuajiri zaidi ya watumishi 4,000 wa sekta ya afya.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameelezea mafanikio yaliyofikiwa kwenye sekta ya maji katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2019 ambapo sh. bilioni 325.9 zimetolewa kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maji ikiwemo uchimbaji wa visima vifupi, vya kati na virefu.
Amesema fedha hizo zimetumika kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama vijijini na mijini. Chini ya utekelezaji wa miradi hiyo, miradi 631 inaendelea kujengwa ikiwemo 558 ya maji vijijini na 73 ya maji mijini.
“Miongoni mwa miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na mradi wa maji Arusha, mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe na mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika miji ya Isaka, Tinde, Kagongwa, Tabora, Igunga, Uyui na Nzega.
Waziri Mkuu ameema lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwahudumia wananchi sambamba na kuratibu vyema utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati. Amesema miradi hiyo inayohusisha sekta ya miundombinu wezeshi, nishati, maji, afya na elimu imekuwa chachu ya kuboresha maisha ya Watanzania kupitia ukuaji wa sekta rasmi na isiyo rasmi.