Home Mchanganyiko WANANCHI MATEMANGA WAFURAHIA KUPATA MAJI YA BOMBA

WANANCHI MATEMANGA WAFURAHIA KUPATA MAJI YA BOMBA

0

Diwani wa kata ya Matemanga halmashauri ya wilaya Tunduru Hamis Kahesa akinawa uso  katika chanzo cha mradi wa maji  Matemanga mara baada ya wakala wa maji vijijini Ruwasa kukamilisha ujenzi wa mradi huo ulianza kujengwa tangu mwaka 2012.

Meneja wa mradi wa watumia maji  wa Matemanga wilaya ya Tunduru Musa Ali akiwaongoza  baadhi ya wakazi wa kijiji cha Matemanga kuchota maji mara baada ya mradi huo kuanza kutoa huduma ya maji ya maji.

Baadhi ya watoto katika kijiji cha Matemanga wakifurahia huduma ya maji ya bomba ambapo kijiji hicho kilikuwa hakijawahi kupata maji ya Bomba tangu Uhuru mwaka 1961.

Picha na Mpiga Picha Wetu,

……………………………………………………………………………………………………….

Na Mwandishi Wetu,Tunduru

KILIO cha muda mrefu cha ukosefu wa maji  safi na salama kwa wananchi wa vijiji vinne vilivyopo kata ya Matemanga wilayani Tunduru,kimepata ufumbuzi kufuatia wakala wa maji vijijini Ruwasa wilaya ya Tunduru kukamilisha mradi mkubwa wa maji Matemanga ulioanza kujengwa tangu mwaka 2012.

Utekelezaji wa mradi huo unamaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa vijiji vya Milonde,Matemanga,Jaribuni na Changarawe ambavyo hapo awali ujenzi wake ulikwama kutokana na mkandarasi wake Kampuni ya M/S Ajax Bulders Ltd kusua sua licha ya kulipwa fedha nyingi na Serikali.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Habarileo baadhi ya wakazi wa kijiji cha Matemanga, wameishukuru  wizara ya maji kukamilisha mradi huo ambao umemaliza kabisa kero ya maji iliyokuwepo kwa muda mrefu na hata kuokoa baadhi ya ndoa  zao.

Sara Kadava, Mwajabu Ali    na Diwani wa kata hiyo Hamis Kahesa walisema,  hapo mwanzo hali ya upatikanaji wa maji katika vijiji vinavyounda kata ya Matemanga ilikuwa mbaya hali iliyoathiri sana shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kilimo ambayo ni uti wa mgongo kwa wakazi hao.

Kadava alisema, mradi wa maji Matemanga ulianza kujengwa  tangu mwaka 2012 lakini umeshindwa kukamilika kwa wakati  na hivyo kuchangia sana wananchi kushindwa kutumia muda wao kufanya kazi za  kujiletea maendeleo badala yake walitumia muda mwingi kufuata maji mbali na makazi yao.

Alisema, kila siku wanawake walilazimika kumka usiku  kati ya saa nane na saa tisa  kwenda mtoni  na kwenye vyanzo vya asili kuchota maji na kurudi saa kumi na mbili asubuhi jambo  lililo changia  kutokea kwa migogo mingi  kwa sababu ya akina mama kuchelewa kurudi nyumbani kutoka kutafuta maji na kuongezeka kwa hali ya umaskini kwa baadhi ya familia.

Ameipongeza Serikali ya awamu ya tano kuvunja mkataba na mkandarasi na kukabidhi  mradi huo kwa wakala wa maji vijijini(RUWASA)wilaya ya Tunduru ambayo imefanikiwa kukamilisha  ujenzi wake  ambao sasa umeanza kuhudumia wananchi.

Mwanahamis Ali alisema,kukamilika kwa mradi huo ni kama ushindi kwa wanawake wa vijiji vyote vinne vya kata ya Matemanga ambao kwa muda mrefu wameteseka kubeba ndoo za maji kichwani na wengine kupoteza ndoa zao kwa kushukiwa kuwa na mahusiano nje ya ndoa zao.

“tulikuwa hatulali kwa kweli,kwani muda mwingi wa kupumzika na waume zetu ndiyo ambao tulilazimika kwenda mtoni na  kwenye vyanzo vya asili kufuata maji,tunaishukuru sana Serikali yetu ya awamu ya tano,tunahaidi tutaiunga mkono na kushiriki katika shughuli zote za maendeleo”alisema, Mwanahamis.

Meneja wa Bodi ya maji Matemanga Musa Mtengela mbali na kuishukuru Serikali kukamilisha mradi wa maji Matemanga alisema, mradi huo ni mkombozi  kwa wananchi ambao kwa muda mrefu walikuwa kwenye mateso  makubwa na sasa unakwenda kuleta tija  na kuharakisha shughuli za maendeleo.

Hata hivyo,ameiomba Serikali kupeleka fedha nyingine ili eneo lililo baki kijiji cha Jaribuni  wananchi wake wafikishiwe mtandao wa maji ya bomba badala ya kuendelea kutumia maji ya visima vya asili ambavyo pia utumiwa  na wanyama kama Tembo na Nguruwe pori.

Kwa upande wake,kaimu Meneja wa Ruwasa wilaya ya Tunduru Batholomeo Matwiga alisema, changamoto kubwa iliyokuwepo katika mradi huo ni uwezo mdogo wa nishati ya umeme jua(solar)kusukuma maji kutoka kwenye chanzo hadi tenki  la kuhifadhia maji.

Kwa mujibu wa  Matwiga, mara baada ya kumuondoa mkandarasi Ruwasa imefanikiwa kuunganisha solar zote 80 kati ya 19 na hivyo kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme  kwenda kwenye mashine za kusukuma maji hadi kwenye tenki.

Alisema,  katika kuhakikisha  kero ya maji katika eneo hilo halitokei tena, wizara ya maji imetoa  milioni 80 ambazo zitapeleka nishati ya umeme wa Tanesco  kwenye chanzo kwa ajili ya kuendesha mashine.

Alisema, baada ya miezi mitatu vijiji vyote vinne  katika kata ya Matemanga kikiwemo Jaribuni vitapata huduma ya maji safi na salama, ambapo amewaomba wananchi wa Matemanga kuhakikisha wanatunza miundombinu  na kutumia maji hayo kwa ajili ya maendeleo.