Diwani wa kata ya Matemanga halmashauri ya wilaya Tunduru Hamis Kahesa akinawa uso katika chanzo cha mradi wa maji Matemanga mara baada ya wakala wa maji vijijini Ruwasa kukamilisha ujenzi wa mradi huo ulianza kujengwa tangu mwaka 2012.
Meneja wa mradi wa watumia maji wa Matemanga wilaya ya Tunduru Musa Ali akiwaongoza baadhi ya wakazi wa kijiji cha Matemanga kuchota maji mara baada ya mradi huo kuanza kutoa huduma ya maji ya maji.
Baadhi ya watoto katika kijiji cha Matemanga wakifurahia huduma ya maji ya bomba ambapo kijiji hicho kilikuwa hakijawahi kupata maji ya Bomba tangu Uhuru mwaka 1961.
Picha na Mpiga Picha Wetu,
……………………………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu,Tunduru
KILIO cha muda mrefu cha ukosefu wa maji safi na salama kwa wananchi wa vijiji vinne vilivyopo kata ya Matemanga wilayani Tunduru,kimepata ufumbuzi kufuatia wakala wa maji vijijini Ruwasa wilaya ya Tunduru kukamilisha mradi mkubwa wa maji Matemanga ulioanza kujengwa tangu mwaka 2012.
Utekelezaji wa mradi huo unamaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa vijiji vya Milonde,Matemanga,Jaribuni na Changarawe ambavyo hapo awali ujenzi wake ulikwama kutokana na mkandarasi wake Kampuni ya M/S Ajax Bulders Ltd kusua sua licha ya kulipwa fedha nyingi na Serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Habarileo baadhi ya wakazi wa kijiji cha Matemanga, wameishukuru wizara ya maji kukamilisha mradi huo ambao umemaliza kabisa kero ya maji iliyokuwepo kwa muda mrefu na hata kuokoa baadhi ya ndoa zao.
Sara Kadava, Mwajabu Ali na Diwani wa kata hiyo Hamis Kahesa walisema, hapo mwanzo hali ya upatikanaji wa maji katika vijiji vinavyounda kata ya Matemanga ilikuwa mbaya hali iliyoathiri sana shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kilimo ambayo ni uti wa mgongo kwa wakazi hao.
Kadava alisema, mradi wa maji Matemanga ulianza kujengwa tangu mwaka 2012 lakini umeshindwa kukamilika kwa wakati na hivyo kuchangia sana wananchi kushindwa kutumia muda wao kufanya kazi za kujiletea maendeleo badala yake walitumia muda mwingi kufuata maji mbali na makazi yao.
Alisema, kila siku wanawake walilazimika kumka usiku kati ya saa nane na saa tisa kwenda mtoni na kwenye vyanzo vya asili kuchota maji na kurudi saa kumi na mbili asubuhi jambo lililo changia kutokea kwa migogo mingi kwa sababu ya akina mama kuchelewa kurudi nyumbani kutoka kutafuta maji na kuongezeka kwa hali ya umaskini kwa baadhi ya familia.
Ameipongeza Serikali ya awamu ya tano kuvunja mkataba na mkandarasi na kukabidhi mradi huo kwa wakala wa maji vijijini(RUWASA)wilaya ya Tunduru ambayo imefanikiwa kukamilisha ujenzi wake ambao sasa umeanza kuhudumia wananchi.
Mwanahamis Ali alisema,kukamilika kwa mradi huo ni kama ushindi kwa wanawake wa vijiji vyote vinne vya kata ya Matemanga ambao kwa muda mrefu wameteseka kubeba ndoo za maji kichwani na wengine kupoteza ndoa zao kwa kushukiwa kuwa na mahusiano nje ya ndoa zao.
“tulikuwa hatulali kwa kweli,kwani muda mwingi wa kupumzika na waume zetu ndiyo ambao tulilazimika kwenda mtoni na kwenye vyanzo vya asili kufuata maji,tunaishukuru sana Serikali yetu ya awamu ya tano,tunahaidi tutaiunga mkono na kushiriki katika shughuli zote za maendeleo”alisema, Mwanahamis.
Meneja wa Bodi ya maji Matemanga Musa Mtengela mbali na kuishukuru Serikali kukamilisha mradi wa maji Matemanga alisema, mradi huo ni mkombozi kwa wananchi ambao kwa muda mrefu walikuwa kwenye mateso makubwa na sasa unakwenda kuleta tija na kuharakisha shughuli za maendeleo.
Hata hivyo,ameiomba Serikali kupeleka fedha nyingine ili eneo lililo baki kijiji cha Jaribuni wananchi wake wafikishiwe mtandao wa maji ya bomba badala ya kuendelea kutumia maji ya visima vya asili ambavyo pia utumiwa na wanyama kama Tembo na Nguruwe pori.
Kwa upande wake,kaimu Meneja wa Ruwasa wilaya ya Tunduru Batholomeo Matwiga alisema, changamoto kubwa iliyokuwepo katika mradi huo ni uwezo mdogo wa nishati ya umeme jua(solar)kusukuma maji kutoka kwenye chanzo hadi tenki la kuhifadhia maji.
Kwa mujibu wa Matwiga, mara baada ya kumuondoa mkandarasi Ruwasa imefanikiwa kuunganisha solar zote 80 kati ya 19 na hivyo kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme kwenda kwenye mashine za kusukuma maji hadi kwenye tenki.
Alisema, katika kuhakikisha kero ya maji katika eneo hilo halitokei tena, wizara ya maji imetoa milioni 80 ambazo zitapeleka nishati ya umeme wa Tanesco kwenye chanzo kwa ajili ya kuendesha mashine.
Alisema, baada ya miezi mitatu vijiji vyote vinne katika kata ya Matemanga kikiwemo Jaribuni vitapata huduma ya maji safi na salama, ambapo amewaomba wananchi wa Matemanga kuhakikisha wanatunza miundombinu na kutumia maji hayo kwa ajili ya maendeleo.