Home Biashara TRA: WAFANYABIASHARA MSIJIHUSISHE NA BIASHARA ZA MAGENDO

TRA: WAFANYABIASHARA MSIJIHUSISHE NA BIASHARA ZA MAGENDO

0

Afisa Msimamizi wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Chama Siriwa akiwaelimisha wananchi wanaofanya shughuli zao katika fukwe ya bahari ya Ununio jijini Dar es Salaam wakati wa kampeni maalum ya kuelimisha wananchi kuhusu athari za magendo katika ukanda wa Bahari ya Hindi.

Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Rose Mahendeka akiwaelimisha wananchi wanaoishi jirani na fukwe ya Bahari ya Kunduchi jijini Dar es Salaam wakati wa kampeni maalum ya kuelimisha wananchi kuhusu athari za magendo katika ukanda wa Bahari ya Hindi.

****************************

Na Veronica Kazimoto
Dar es Salaam
 
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wafanyabiashara na wachuuzi wanaoishi jirani na fukwe za Bahari ya Hindi kutojihusisha na biashara za magengo
kwani kufanya hivyo ni kuisababishia nchi kukosa mapato yake stahiki kutokana na wahusika wa biashara hizo kukwepa kulipa kodi.

 

Akizungumza na wafanyabiashara hao katika fukwe za bahari za Msasani, Mbweni, Ununio, Beach kidimbwi na Kunduchi zilizopo jijini Dar es Salaam, Afisa Msimamizi
Mkuu wa Kodi, Rose Mahendeka, kutoka Mamlaka hiyo ameeleza kuwa, watakaobainika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kukamata bidhaa zote na kutaifisha vyombo vilivyohusika kubeba bidhaa hizo.

 

“Tumeamua kufanya kampeni maalum ya kuelimisha wananchi kuhusu athari za magendo katika ukanda wa Bahari ya Hindi na moja ya madhumuni ya kampeni hii ni
kuwaonya wale wote wanaojihusisha na biashara za magengo kwani adhabu yake siyo tu kukamata bidhaa na kutaifisha vyombo bali pia kuchukuliwa hatua za kisheria
ikiwemo kufungwa jela,” alisema Mahendeka.

 

Ameongeza kuwa, mbali na wahusika hao wanaojihusisha na biashara za magendo kukwepa kulipa kodi ya Serikali, kuna uwekezekano wa kuwasababishia wananchi
madhara ya kiafya kwa kuwa bidhaa zinazopita katika njia zisizo rasmi zinakuwa hazijathibitishwa na Mamlaka husika za Serikali. 

 

“Ni muhimu tukumbuke kwamba, bidhaa zote zinazopita katika njia za vichochoro au bandari bubu hazipiti katika utaratibu rasmi na hivyo zinakuwa hazijakaguliwa wala
kuthibitishwa kama ni salama au la na Mamlaka husika kama vile TBS, TMDA, Mkemia Mkuu wa Serikali na nyinginezo. Kwa mantiki hiyo, bidhaa hizo zinaweza kuhatarisha afya za walaji,” alieleza.

 

Kampeni ya kuelimisha wananchi kuhusu athari za magendo katika ukanda wa Bahari ya Hindi imeanzia mkoa wa Dar es Salaam na timu ya maafisa wa TRA wanaendelea
na kampeni hiyo katika mikoa ya Pwani, Tanga, Mtwara na Lindi.